Dar Bodaboda Super Star #Unity Festival kufanyika Mei 13, zaidi ya bodaboda 5,000 kushiriki

0
211

Kufuatia usafiri wa bodaboda kuongoza kwa usababishaji wa ajali barabarani zinazopelekea watu wengi kupoteza maisha na au kuwa walemavu wa kudumu, pamoja na kuhusishwa na matukio ya uhalifu hapa nchini.

Kampuni ya JP Decaux na Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na masuala ya maendeleo katika jamii IRI, wameandaa tamasha maalumu kwa wadau wa sekta ya bodaboda linaloitwa ‘DAR BODABODA SUPERSTAR UNITY FESTIVAL’ ambalo limelenga kutoa semina za umuhimu wa uendeshaji ulio salama kwa kuzingatia sheria za barabarani na umuhimu wa matumizi ya bima.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa kampuni ya JP Decaux Ltd, Bwana Shaban Makugaya amebainisha kuwa, zaidi ya waendesha bodaboda 5,000 kutoka Wilaya zote za Dar es Salaam watajumuika pamoja kushiriki tukio hilo ili kumpata mshindi mmoja ambaye atakuwa ndio Star wa Bodaboda wa Dar.

“Tumefuata kundi ili la waendesha bodaboda kwani halina muingiliano wa kidini wala siasa. Hivyo kupitia tamasha ili mshindi atapatikana mmoja pekee” alieleza Shaban Makugaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa JP Decaux Ltd, Bwana Elias Richard amebainisha kuwa, mbali na kumtafuta mshindi, pia washiriki wote watapata fursa ya kufundishwa semina elekezi ya usalama barabarani na majukumu yao ya wawapo barabarani huku pia wakitarajiwa kupata burudani kali kutoka kwa wasanii mbalimbali wa muziki hapa nchini.

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Mei 13.2017 katika viwanja vya Tanganyika Packers vilivyopo Kawe Jijini Dar es Salaam huku pia kukitarajia kuwa na michezo tofauti kama vile mashindano ya mbio fupifupi kwenye mchanga, matope na kuendesha kwenye vikwazo.

“Lengo la tamasha hili ni kuweka uamsho na msisitizo wa wa utolewaji wa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa pikipiki na abiria kwa dhumuni la kuzingatia sheria za usalama barabarani. Pia limelenga kudumisha umoja na ushirikiano katika jamii” walieleza.

Tamasha hilo litakuwa ni la kila mwaka  huku idadi ya washiriki nayo ikiwa inatarajia kuongezeka zaidi.

  Tazama BongoNews TV kuona zaidi tukio hilo hapa

DAR BODABODA SUPERSTAR UNITY FESTIVAL

Meneja Mkuu wa kampuni ya JP Decaux Ltd, Bwana Shaban Makugaya akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani)

Meneja Mkuu wa kampuni ya JP Decaux Ltd, Bwana Shaban Makugaya akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) wakati wa kutoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari mapema leo Aprili 27.2017, Jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa JP Decaux Ltd, Bwana Elias Richard.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here