Kliniki ya Afya ya Akili kutolewa kupitia Hospitali zote za Rufaa nchini- Dk.Kigwangalla

0
286

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dkt. Khamisi Kigwangalla amekutana na  viongozi wa Chama Cha Walemavu wa Afya ya Akili (TUSPO), waliomtembelea Bungeni jana  Mei 22.2017, Bungeni Dodoma.

Viongozi hao walikaribishwa na Wabunge wawakilishi wa Watu wenye changamoto mbali mbali za ulemavu nchini,  Mhe. Amina Mollel (Mb.) na Mhe. Stella Ikupa (Mb.). Katika kikao hicho Dkt. Kigwangalla ameweza kujadiliana nao mambo mbalimbali viongozi hao wa TUSPO  ikiwemo uanzishwaji wa Kliniki ya Afya ya Akili kupitia Hospitali zote za Rufaa za Mkoa hapa nchini.

“Nimekutana na Viongozi wa TUSPO ambao  wanashughulika na masuala ya Afya ya Akili. Tulijadili mambo mengi na niliwaelezea mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwenye eneo hili, ikiwemo Uanzishwaji wa Kliniki za Afya ya Akili kwenye Hospitali zote za Rufaa za Mkoa nchini nzima. Lakini pia Uanzishwaji wa Rehabilitation Centers kwenye kila kanda na usambazaji wa Madaktari bingwa wa Afya ya Akili na wataalamu wote wanaohitajika kutoa huduma hizi kwenye Hospitali na vituo hivi” Ameeleza Dkt. Kigwangalla.

Aidha, ameongeza kuwa, amewaahidi uongozi huo wa TUSPO,  kuwa atafuatilia juu ya hatua ambayo mchakato wa kukamilisha muundo wa kisheria (legal framework) ulipofikia na sababu za kukwama kwake toka sheria ya afya ya akili ilipotungwa mwaka 2008.

“Serikali ya awamu ya tano ni sikivu kwa wananchi wake bila kubagua. Nina aahidi kulifuatilia sualala uanzishwaji wa Baraza la Afya ya Akili, kwani  tayari sheria ilishatungwa muda mrefu. Na kwamba ni kwa nini Baraza la Afya ya akili halijaanzishwa toka sheria itungwe mpaka leo na kwa nini mpaka leo hakujawa na kanuni za Afya ya akili kuelekeza juu ya mambo mbalimbali” alieleza Dkt. Kigwangalla ambapo amewaahidi kuwapa taarifa ya utekelezaji wa masuala hayo kwenye Bunge la  Mwezi November 2017.

Kuhusu Magonjwa ya Akili Tanzania:

Magonjwa ya akili ni magonjwa ambayo yanaathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda, na hivyo kuwa na tabia au mwenendo uliotofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila, desturi, na nyanja nyingine za kijamii. Tabia hizo zinatokana na ugonjwa wa akili kuathiri ufanisi na shughuli za mtu husika (mgonjwa) au huathiri jamii nzima inayomzunguka endapo mgonjwa huyo hatopatiwa matibabu stahiki na kwa wakati muafaka.

Kwa Tanzania imeeelezwa kuwa baadhi ya wagonjwa wengi wa akili hawafiki katika vituo vya kutolea huduma za afya na badala yake kuishia kwenye tiba za jadi au kutelekezwa na kunyanyapaliwa huku takwimu za zinaonyesha kuwa Tanzania ina idadi ya watu takriban milioni 45 na kutokana na taarifa ya afya ya akili kwa mwaka 2014/15 inaonyesha kuwa idadi ya watu 817,532 wanaugua magonjwa mbalimbali ya akili nchini, hii ni karibu asilimia 2 ya watanzania wote.

Pia idadi hii ni ongezeko la wagonjwa 367,532 ukilinganisha na takwimu za mwaka 2013/14 walikuwa ni 450,000. Kati ya wagonjwa wote wa akili kwa mwaka 2014/15 wanawake ni ni 332,000 na wanaume ni 485,532.

Mkoa wa Dar-Es-Salaam unaongoza kwa kuwa n awagonjwa wengi nchini ukifuatiwa na mkoa wa Dodoma na mkoa wa mwisho ni Lindi. Idadi hiyo ya wagonjwa ni wale walioweza kuhudhuria katika vituo vya kutolea huduma ya afya hapa nchini.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dkt. Khamisi Kigwangalla akifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Walemavu wa Afya ya Akili (TUSPO), waliomtembelea Bungeni jana  Mei 22.2017, Bungeni Dodoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here