Dk. Kigwangalla: “Serikali tumechukua hatua za haraka za kumsaidia Mzee aliyechora nembo ya Taifa”

0
246

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ,Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla mapema leo amemtembelea na kumjulia hali,  mchoraji  wa Nembo ya Taifa , Mzee Francis Maige Kanyasu zadi ya 80, ambaye alilipotiwa hivi karibuni na baadhi ya vyombo vya habari namna anavyoishi huko nyumbani kwake Buguruni, Malapa.

Akuzungumza na waandishi wa habari wakati wa tukio hilo alipoenda kumtembelea Mzee huyo ambaye awali alikuwa amelazwa Amana kwa matibabu, Dk. Kigwangalla alimtembelea Hospitalini hapo ambapo alimjulia hali na mambo mengine ambapo aliagiza kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo tayari anaendelea na vipimo kwenye hospitali hiyo ya Taifa.

Imeelezwa kuwa, awali Mzee Kanyasu alipelekwa Hospitali ya Amana na baadhi ya majirani zake hata hivyo, Naibu Waziri wa Afya Dk. Kigwangalla lipofika kumtembelea Hospitalini hapo alibaini kuwa anahitaji matibabu na vipimo zaidi hivyo kuamuru apelekwe Hospitalini hiyo ya Muhimbili.

 Akiulizwa na vyombo vya habari namna ya hatua waliyochukua kama serikali, Dk ameeleza kuwa, baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari, wamefuatilia na kuchukua hatua kwani awali hawakuwa na taarifa nae.

“Kwa sasa tumeamua kuanza na hatua za kumpatia matibabu  ya haraka.  Lakini pia baada ya matibabu tutachukua jukumu la kumpatia sehemu ya malazi na makazi maalum ya Wazee  pamoja na mambo mengine. Lakini pia baada ya hatua zote pia tutaangalia taratibu zingine endapo atarejea mahala alipopazoea ama katika makazi maalum ya Wazee” amesema Dk. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mzee huyo anasema kuwa,  miongoni mwa mambo yanayomsumbua ni pamoja na suala la kutotembea vizuri.

Awali akimwelezea Naibu Waziri wa Afya. Dk. Kigwangalla, Mzee huyo amesema kuwa, Buguruni Malapa mahala alipokuwa akiishi alikuwa amepanga lakini baadae baada ya kushindwa kulipa aliweza kupewa ofa ya kuishi bure kwa hisani ya majirani ambao inaelezwa ameishi  nao vizuri tokea mwaka 1977.

“Nipo hapa tokea 1977,  nikiwa na Mke wangu tukitokea Bulima, Misungwi na kufikia nyumba hii ninayoishi  hadi sasa. Shule nimesomea huko Misungwi” ameeleza Mzee huyo.

Ameongeza kuwa, alizaliwa  mwaka  1931, Lakini hakubahatika kupata motto yoyote akiwa na mkewe ambaye bahati mbaya alifariki  na kubaki pekee yake.

Aidha, katika suala la kuumwa, anabainisha kuwa,  ndugu zake hawajui kama anaumwa, lakini wanafahamu kuwa anaishi Buguruni Malapa.

Awali amefafanua kuwa, aliweza kuchora nembo hiyo   mwaka 1957, wakati huo aliambiwa nembo hiyo Uhuru ukipatikana itazunguka nchi nzima, Ambapo aliweza kuchora akiwa na mwenzake ambaye kwa sasa ni marehemu, aliyefahamika kwa majina ya Alipanga Mazanga kutoka Pangani, Mkoani Tanga. Hata hivyo Mzee huyo anasema yeye kazi yake ni kuchora tu ndio kipaji chake pekee.

Dk. Kigwangalla amevipongeza vyombo vya habari kwa kuripoti taarifa ya Mzee huyo kwani imeweza kuwawezesha wao kama Serikali kuchukua hatua za haraka kwani awali hawakuwa wanafahamu juu ya Mzee huyo.

“Niseme tu kama Serikali tunavipongeza vyombo vya Habari kwa kuweza kutoa habari za Mzee wetu huyu na awali hatukuwa na taarifa yake hivyo kwa kuwa Serikali yetu ni sikivu, tumechukua jukumu la kumsaidia masuala yote ikiwemo hatua hii ya sasa ya kumpatia matibabu na uchunguzi wa kina nan baada ya hapo ataweza kupata makazi maalum yaliyo chini ya Serikali.” Amemalizia Dk. Kigwangalla.

Naibu Waziri Dkt.Kingwagalla akiongea na waandishi wa habari kuhusu hatua waliyochukua ya kumuhamishia Mzee Maige kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili

Naibu Waziri Dkt.Kingwagalla akimjulia hali Mzee Kanyasu wakati alipomtembela Hospitali ya Amana ambapo aliagiza apelekwe Muhimbili kwa uchunguzi zaidi. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here