Shida ya maji Mwera kiongoni kuwa historia

0
100

Shida ya maji inayowakabili wananchi wa kijiji cha Mwera Kiongoni, inatarajiwa kuwa historia baada ya wiki chache zijazo.

Matumaini ya kumalizika kwa kero hiyo yamekuja kufuatia Mwakilishi wa jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said kukabidhi mipira sita ya kusambazia maji iliyogharimu shilingi 2,500,000.

Kwa miaka mingi, wananchi wa eneo hilo lenye historia kubwa kwa kuwa ndiko alikozaliwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume, wamekuwa wakitumia maji ya visima ambayo hayana uhakika wa usalama.

Akizungumza kwa niaba yake na Mbunge wa jimbo hilo Khalifa Salum Suleiman wakati wa makabidhiano hayo, Mwakilishi Simai alisema msaada huo ni miongoni mwa malengo yao ya kuwaondoshea wananchi shida mbalimbali zinazowakabili hatua kwa hatua.

Alisema baada ya kupokea taarifa kutoka uongozi wa wadi ya Ubago juu ya tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama, na sasa wanaanza harakati za kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi.

Alifahamisha kuwa baada ya kutandikwa mipira hiyo ikiwa awamu ya kwanza, juhudi zitaendelea kufikisha maji kutoka Kwa kozi hadi Mkorogo, ili kuhakikisha viambo vyote vinapata maji kutoka masafa ya karibu.

Hata hivyo, aliwakumbusha wananchi wahakikishe kuwa mipira hiyo hawaitandiki karibu na hifadhi ya barabara, akisema iko katika mipango ya serikali kuitengeneza, kwani nayo ni miongoni mwa kero za muda mrefu zinazowakabili wanakijiji wa huko.

“Mbali na hapa, pia tuko katika juhudi za kuhakikisha maeneo yote ya jimbo letu la Tunguu yanaondokana na shida ya maji, hivyo tunaiomba Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ituunge mkono,” alisema Simai.

Alitoa wito kwa vijana wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi wakati wa kuchimba msingi utakaotandikwa mipira hiyo ili hatimaye maji yaweze kupatikana kirahisi.

Naye Diwani wa wadi ya Ubago Ussi Ali Mtumwa, alisema baada ya kupata mipira hiyo, sasa ni kazi tu, na kutaka wananchi wapange siku ya kuanza shughuli na kuimaliza haraka ili kutoa nafasi ya kuendelea na hatua nyengine.

Alisema mbali na changamoto ya maji, pia wanahitaji kujengewa barabara kwa kiwango cha lami, kwani kwa sasa iko katika hali mbaya.

Mmoja kati ya akinamama wa eneo hilo Tamaduni Ibrahim Maulid, alisema hatua ya Mwakilishi na Mbunge kuwapelekea msaada huo, itawaondoshea shida ya kutumia maji ya visima yasiyokuwa na uhakika wa usalama kiafya.

“Kijiji chetu cha Mwera Kiongoni kina shida kubwa ya maji, na kwa kweli tumechoka kuhangaika na madoo visimani, mara nyengine tukiwa na watoto migongoni, na vifua vinaumia. Tunashukuru sasa Mwakilishi na Mbunge wamesikia kilio chetu,” alifafanua. 

Hata hivyo, kwa niaba ya wananchi wenziwe, alisema iko haja serikali ifikirie mpango wa kuijenga barabara hayo ambayo alieleza kuwa iko katika hali mbaya na gari zinashindwa kufika huko na kuishia kwa Kozi, ambayo ni masafa marefu hadi katika kijiji chao.

Mwakilishi wa jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said (katikati), akiwa amekaa na baadhi ya wananchi wa jimbo lake kabla ya kukabidhi mipira ya kusambazia maji kwa wananchi wa kijiji cha Mwera kiongoni jimboni mwake.

Mwakilishi wa jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said (katikati), akikabidhi mipira ya kusambazia maji kwa wananchi wa kijiji cha Mwera kiongoni jimboni mwake, kwa ajili ya kuwasogezea huduma ya maji safi na salama na kuondokana na matumizi ya maji ya visima.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here