Tujikumbushe hotuba ya Zitto Kabwe Bungeni mwaka 2009

0
813

HOJA YA KUJADILI TAARIFA YA KAMATI YA BOMANI BUNGENIKikao cha Pili cha Bunge|Oktoba 29, 2008

Mheshimiwa Naibu Spika,

Nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.  Kwanza, naomba niseme kwamba, nilikuwa mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Rais ya kushughulikia suala la Sekta ya Madini, kwa hiyo ninaomba ni-declare interest kabisa.

Pili, napenda kupokea pongezi ambazo Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imezitoa kwa Kamati ya Rais chini ya Uenyekiti wa Jaji Bomani.  Wenzangu wote hawapo, kwa hiyo, kwa niaba ya wenzangu walio Wabunge na wasio Wabunge, napenda kuishukuru sana Kamati na pia Waziri kwa pongezi ambazo amezitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika,

Binafsi naomba kuwashukuru sana Wajumbe wote wa Kamati, sitaweza kuwataja majina kwa sababu ya muda.  Zipo nyakati ambazo zilikuwa ngumu sana kwa sababu tulikuwa tuna watu ambao wapo Serikalini, lakini baadae tuliweza kuweka maslahi ya taifa letu mbele na kuweza kufikia Ripoti hii ambayo tumeitoa, ambayo Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeonyesha kwamba ni Ripoti nzuri sana.

Pili, binafsi napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais si tu kwa kuunda Kamati ile bali kwa kuniteua. Kwa sababu alinipa fursa ya kuweza kuijua Sekta ya Madini na kuweza kutoa mchango wangu katika maendeleo ya taifa letu.  Namshukuru sana Mheshimiwa Rais na kama hasikii, Mheshimiwa Waziri Mkuu atampelekea shukrani zangu, hasa ukizingatia kwamba Rais aliniteua katika Kamati hii nikiwa nimesimamishwa Ubunge.  Kwa hiyo, ilikuwa ni heshima kubwa sana kwangu kwa yeye kuweza kuniteua.  (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,

Niungane na wasemaji wawili waliopita kuhusiana na nafasi ya Sekta ya Madini katika uchumi wa taifa letu.  Sekta hii imekuwa ni moja ya sekta ambazo zinakua kwa kasi sana.  Kati ya mwaka 2000 – 2006, Sekta ya Madini ilikuwa kwa wastani wa asilimia 15; mwaka jana sekta hii imekua kwa asilimia 10 na imeshuka kwa sababu mgodi wa Buhemba ulifungwa na vilevile hapakuwa na uwekezaji mpya ambao umepatikana baada ya kuwa migodi mingine yote imeshaanza uzalishaji.

Sekta hii inachangia asilimia 44 ya mapato ya mauzo ya nje ya taifa letu, lakini inachangia asilimia 3.5 ya pato la taifa. Sasa hapo ndipo swali hasa na kitendawili kinapokuja; inakuwaje sekta inayokua sana na inayochangia takriban nusu ya mauzo yetu nje, inachangia kidogo sana katika pato la taifa?  Jibu rahisi ni kwamba, Sekta ya Madini ipo mbali sana na sekta nyingine za uchumi.  Katika jambo ambalo Serikali lazima iliangalie kwa kina ni jinsi gani ya kuhakikisha kwamba Sekta ya Madini inakuwa na mahusiano na sekta nyingine za kiuchumi.

Taarifa ya Hali ya Umaskini Nchini (Poverty and Human Development Report) ya mwaka 2007, naomba ninukuu inasema:  “There is no indication that expansion in mining has triggered significant growth in local economies or influenced poverty reduction.”  Hii ni kwa sababu ya lack of forward and backward linkages.

Mheshimiwa Naibu Spika,

Leo huwezi kusema toka tumeanza uwekezaji kwenye Sekta ya Madini ni kiasi gani imeweza ku-stimulate ukuaji katika sekta kwa mfano ya kilimo. Ni vipi ambavyo wakulima wanaotoka maeneo ambayo yana madini wanafaidika moja kwa moja na uwekezaji mkubwa? Mlisikia lawama mbalimbali za wananchi kuhusiana na makampuni ya madini kuagiza hata nyanya kutoka nje, kitu ambacho kwa miaka miwili iliyopita sasa kimebadilika. 

Kumekuwa na baadhi ya maeneo, kwa mfano, Kahama ambapo sasa akina mama wameanza shughuli za bustani kwa ajili ya kuweza kufanya ugavi wa baadhi ya vyakula kwenda katika migodi, lakini kuna baadhi ya maeneo bado ni tatizo; kwa mfano, nyama mpaka sasa migodi takriban yote Tanzania inaagiza nyama kutoka Kenya.

Nyama inayoagizwa kutoka Kenya ni ng’ombe ambao wamenunuliwa Tanzania, yaani Wakenya wamekuja kununua ng’ombe Tanzania wakaenda kwenye machinjio yao wakauza, waka-park, wakarudisha Tanzania.  Kwa hiyo, hili ni suala ambalo ni lazima tuliangalie na kuweza kuona ni vipi ambavyo Sekta ya Madini inahusiana na sekta nyingine.

Hatuwezi kufaidika na madini kwa kodi peke yake, haiwezekani. Mnaweza mkakusanya kodi mtakavyo, lakini bado impact yake kwenye ukuaji wa uchumi mpana haitaonekana. Njia pekee ya kufaidika na ukuaji na Sekta ya Madini ni kuhakikisha kwamba, sekta nyingine za uchumi zinaendana na Sekta ya Madini.  Hapa tuna mfano mzuri sana wa umeme; lawama ambazo tunazo sasa hivi, tunapoteza fedha nyingi sana kwa kuwasamehe kodi wawekezaji kwa sababu ya kuagiza mafuta ya kuzalisha umeme.  (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,

Geita peke yake wakizalisha kwa kiwango cha asilimia mia moja, wanahitaji takriban megawatt 37 za umeme.  Kanda ya Ziwa kwa ujumla wake na kama uzalishaji wa Kabanga Nickel ukianza, tutahitaji Megawatt 200 za umeme kwa ajili ya Kanda ile tu kwa Mkoa wa Shinyanga, Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Mwanza.

Kwa hiyo, lazima tunapokuwa tunapanga tuweze kuangalia tunaisaidia vipi TANESCO iweze kupeleka umeme kule, kwa sababu hili ni soko ambalo lipo tayari na hapo ndipo unapokuja kwenye hoja nzima ya kuangalia kwamba katika Kanda ya Ziwa wenzetu wanafanya nini.

Mheshimiwa Naibu Spika,

Leo Rwanda wana gesi yao ile methanol, wana mpango wa kuzalisha megawatt 300 za umeme.  Rwanda peke yake hata ikiwa industrialized namna gani, haitazidisha kutumia megawatt 150 kwa sababu sasa hivi wanatumia megawatt 38 mpaka 40 za umeme. 

Kwa maana hiyo ni kwamba, tayari Rwanda wameshaona kuna soko Kabanga Nickel kwa ajili ya umeme.  Kwa hiyo ni lazima tuweze kupanga mambo yetu kwa kuangalia na upana wake na ndiyo jinsi ambavyo sekta hii itaweza kutusaidia.

Kuna mambo ambayo ningependa Waheshimiwa Wabunge wayatilie mkazo kiasi chake; kwa mfano, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, imependekeza kufanya uchunguzi maalum kuhusu uuzaji wa hisa za Mgodi wa Bulyanhulu. Mheshimiwa Dkt. Chegeni amezungumzia hisa za Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika,

Bulyanhulu ulikuwa ni Mgodi wetu uliokuwa unamilikiwa na STAMICO.  Tukaiondoa STAMICO katika kufanya shughuli yoyote ile.  Hisa asilimia 85 wakapewa Kampuni ya Sutton Resources, asilimia 15 wakabaki nayo STAMICO, ambayo ikawa chini ya Msajili wa Hazina.

  Kampuni ya Sutton Resources ikawekeza Dola milioni 20 katika Mgodi ule.  Miaka mitatu baadae wakauza Mgodi wa Bulyanhulu kwa Kampuni ya sasa ya Barrick kwa Dola milioni 348.  Mtu ambaye amewekeza Dola milioni 20, kapata ziada Dola milioni 328. Serikali ya Tanzania haikupata kodi hata senti tano kwa sababu zote hizi ziliuzwa kupitia Soko la Hisa la Toronto.

Mheshimiwa Naibu Spika,

Naiunga mkono kabisa Kamati ya Nishati na Madini kuamua kufanya uchunguzi maalum, kwa sababu hata jinsi tulivyouza hizo hisa asilimia 15 zilizobakia, kunatia mashaka makubwa sana.  Hisa asilimia kumi tulizi-exchange na sheria ya kodi kuhusu Withholding Tax kwamba, hatutapata Dividend, kwa hiyo ni bora tupate Withholding Tax.  With-holding Tax hatupati, hiyo Dividend haijawahi kutangazwa kwa sababu Bulyanhulu hawajapata faida. Kwa hiyo, hiki ni kitu ambacho ningependa Kamati iweze kukiangalia, isiiangalie Bulyanhulu peke yake.

Kamati ya Nishati na Madini ikitaka kufanya uchunguzi ulio kamili, ifanye uchunguzi wa Mgodi wa Buhemba, pale ndio kuna tatizo kubwa sana. Kuna tatizo kubwa kwa sababu si tu Mwekezaji wa Buhemba ameondoka bila kulipa wafanyakazi, bila kufanya taratibu za kufunga Mgodi, kuathiri mazingira, Wananchi wa Buhemba sasa hivi wana matatizo makubwa ya vyanzo vya maji, kwa sababu ya yule Mwekezaji.

  Vilevile kuna fedha ambazo sisi tuliwapa wale wawekezaji, ndiyo hiyo mnayosikia kashfa ya Meremeta. Kamati yetu imeonyesha katika taarifa yake kwamba, tumeshindwa kufahamu ni nini hasa kilitokea katika umiliki wa Mgodi wa Buhemba na uhusikaji wa Kampuni ya Meremeta.

Mheshimiwa Naibu Spika,

Kwa hiyo, kuna haja kubwa sana; naliomba Bunge lako Tukufu, wakati Kamati ya Bunge ya Madini inafanya uchunguzi kuhusiana na mazingira ya Bulyanhulu, wafanye uchunguzi pia kuhusiana na mazingira ya Mgodi wa Buhemba.  Wakati huo huo Serikali kwa haraka iwezekanavyo, ilipe mafao yanayostahili wale wafanyakazi wa Buhemba ambao mpaka sasa bado hawajalipwa. Vilevile kuna malalamiko katika Mgodi wa Bulyanhulu kuhusiana na jinsi gani ambavyo wananchi waliondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika,

Njia pekee ya kuondoa mashaka ya kwamba malalamiko haya ni sawa ama si sawa ni kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kufanya uchunguzi maalum, kwa sababu kuna watu walikuja kwenye Kamati ya Mzee Bomani, wakajieleza wazi wazi kwamba ndugu zao walifukiwa kwenye mashimo, lakini mpaka leo hakuna uchunguzi wa Kiserikali ambao ulifanyika.

Kwa hiyo, ningependa pia Kamati ya Nishati na Madini katika uchunguzi wake, ihusishe uchunguzi kuhusiana na kama kweli kuna wananchi ambao walifukiwa katika mashimo pale Bulyanhulu na kuweza kuona hatua gani ambazo tunaweza kuzichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika,

La mwisho ni role yetu; ningependekeza ifikie wakati, inapokuja Miswada ambayo ni ya kitaalam sana, Kamati za Bunge ziruhusiwe kuajiri Consultants kwa ajili ya kufanya Impact Study ya ule Muswada, kwa sababu leo tunapozungumza tunapoteza kodi kwenye Migodi ni kwa sababu ya Sheria ambazo tumezipitisha sisi wenyewe.

Sheria ambayo Mheshimiwa Shellukindo ameizungumza hapa kuhusiana na ile asilimia 15, Clause ambayo tumeitoa tukairudisha na tulibishana hapa sana wakati wa hoja ya Buzwagi kuhusiana na hiyo Clause.

Mheshimiwa Naibu Spika,

Sheria hii TRA wametufahamisha katika kipindi cha miaka 10 iliyopita tumepoteza Dola milioni 883 kwa kodi ambayo imeshindwa kukusanywa, kwa sababu ya kipengele hiki cha sheria ambacho tulikipitisha ndani ya Bunge.  Kwa hiyo, kuna haja kubwa sana, maana haya ni makosa tumeshayafanya, hata tufanye nini makosa yameshafanyika;

cha msingi ni kuweza kuangalia mbele kuona ni jinsi gani ambavyo makosa kama haya hayajirudii kwa sababu tunakwenda kwenye gesi, tunakwenda kwenye mafuta, kuna Migodi mingine zaidi inakuja, kuna Mkataba Mpya unatakiwa kusainiwa wa Kabanga Nickel, Mwanza tena wamegundua Nickel nyingine, Kigoma Kijiji cha Mwamgongo wamegundua Nickel na baadhi yao wamegundua Uranium. Mikataba hii itakapoingiwa, kama hatujaweza kuwa tumejiwekea utaratibu ambao Kamati za Bunge zitaweza kupata ushauri wa kitaalam, tunaweza kujikuta tunarudia makosa ambayo tuliyafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika,

La mwisho kabisa, kama nitatumia dakika mbili za mwisho ni kuhusiana na suala la Ring Fencing, Mzee Shellukindo amelizungumza. Ningependa kutoa mfano dhahiri ili Wabunge waweze kufahamu na wananchi pia waweze kuona.  Suala la Mgodi wa Tulawaka unaomilikiwa na Kampuni moja na Kampuni hiyo hiyo ndiyo inayomiliki Mgodi wa Buzwagi.

Ukisoma Ripoti hii ya Kamati ya Rais, utagundua kwamba fedha ambazo zilikuwa zilipe kodi Tulawaka, ndiyo zimejenga Buzwagi. Rekodi zetu zinaonyesha kwamba, Investment ya Buzwagi ya 400 million USD imeletwa na Pangea Minerals, ambayo ni Kampuni Tanzu ya Barrick. Ukiisoma hii Ripoti unagundua kwamba, kwa sababu ya ukosefu wa Ring Fencing, gharama za ujenzi wa Buzwagi zilikuwa zinaingizwa Tulawaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda umekwisha nakushukuru sana.

Naunga mkono mapendekezo ya Kamati ya Rais na Mapendekezo ya Kamati ya Nishati na Madini.  (Makofi)

(Mwisho wa hotuba)

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here