Rais Magufuli afungua Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba)

0
130

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wadau wa maendeleo zikiwemo kampuni za biashara za ndani na nje ya nchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini na ametoa wito kwao kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika viwanda.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 01 Julai, 2017 katika hotuba yake ya ufunguzi wa Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Dkt. Magufuli ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuboresha uwekezaji katika viwanda ikiwemo masuala ya kodi na kuongeza uzalishaji wa umeme na ameahidi kuwa wote watakaokuwa tayari kujenga viwanda watapata ushirikiano wa kutosha kufanikisha azma hiyo.

“Tunapanua mradi wa Kinyerezi I na tunajenga Kinyerezi II na III, hizi zote zitatupatia Megawatts 600 za umeme, na pia tumeamua kutekeleza mawazo ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya kujenga mradi wa umeme katika maporomoko ya maji ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), mradi huu utatupatia Megawatts 2,100.

“Ni mradi mkubwa na tumeamua kuanza kuujenga kwa kutumia fedha zetu, najua watu watajiuliza fedha tutapata wapi, nasema tutajenga” amesema Mhe. Rais Magufuli na kusisitiza kuwa licha ya manufaa ya kupata umeme pia bwawa litakalojengwa litatumika kwa uvuvi, maji ya wanyamapori na Kilimo.

Mhe. Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage kuongeza muda wa maonesho hayo kwa siku 5 zaidi ambazo zitaishia tarehe 13 Julai, 2017 ili Watanzania wapate muda mwingi zaidi kutembelea na kujifunza teknolojia, ujuzi na mbinu mbalimbali za biashara.

Mhe. Dkt. Magufuli amezipongeza kampuni 515 kutoka nchi za nje 30 na kampuni zaidi ya 2,500 za ndani ya nchi zinazoshiriki katika maonesho hayo makubwa Afrika Mashariki na Kati na ametembelea baadhi ya mabanda ya kampuni hizo.

Gerson Msigwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

01 Julai, 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipungia mkono wananchi wakati akitembelea mabanda mbalimbali baada ya kufungua rasmi maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam leo. 

Rais Magufuli ameyafungua rasmi Maonyesho hayo, yaliyoanza Juni 28 – Julai 8, 2017, ambapo kwa ushauri wake, Maonyesho haya kwa mwaka huu yameongezewa siku tano zaidi na kutarajiwa kumalizika Julai 13, 2017. Picha na Ikulu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here