‘Millennials’, Teknohama na kesho ya Tanzania yangu

0
92

Nilipoamka kufanya ibada zangu za usiku na kula daku kabla sijainuka nikakamata simu nione kilichojiri, haswa baada ya kupitiwa na usingizi bila taarifa kwa sababu ya uchovu jana yake. Maana mara nyingi huwa najizuia kugusa simu usiku. Sababu nikigusa tu basi usingizi hupaa! Nitaingia kwenye meseji za kawaida, ambazo siku hizi hazibambi sana na si nyingi haswa kama zamani; kisha nitaingia kusoma meseji za ‘Whatsapp’; pia nitatamani kupita kule kwenye mtandao wa ‘mapicha picha’ ujulikanao kama ‘Instagram’, kwenye ukurasa wangu wa ‘Facebook’ na baadaye ‘Twitter’.

Mpaka nikamalize kuperuzi kote huku na asubuhi itakuwa imefika. Siku hizi ukitaka usilale pitia huku, ukitaka kulala, basi wewe kamata kitabu chako tu, hata kiwe na simulizi nzuri namna gani, nakuhakikishia utasinzia tu!

Nilipofika Facebook, ambapo jana yake nilikuwa nimebandika makala yangu ya kisiasa niliyokuwa nimeituma kwenye gazeti la Raia Mwema, nikakutana na michango (comments) kibao ya wasomaji wangu. Makala yangu ilikuwa ikihusu uzalendo, kujitoa kwa ajili ya nchi yetu na kuhusianisha haya na uchapakazi wa Rais Magufuli na matokeo chanya yanayokuja na uongozi wake thabiti n.k.

Nikakutana na michango mchanganyiko sana; mingi ikiunga mkono kazi ya Rais wetu, mingine ikiendelea kupaza sauti za malalamiko. Nikapata hisia kuwa wengi wa wachangiaji wa mada yangu ni vijana wa kizazi kipya, wenyewe wanapenda wajulikane kama ‘watoto wa kizazi cha kuhoji’ ama ‘watoto wa zama za kidijitali’; nikakumbuka wakati nasoma somo la takwimu kwenye digrii yangu ya tatu nilifundishwa

kundi la kizazi cha zama za kukua kwa teknohama maalum kama ‘millenials’ ama wanatakwimu wengine wanawaita ‘Generation Y’ ama ‘Echo boomers’, kuwatofautisha na wale ‘baby boomers’ waliozaliwa baada ya vita ya pili ya dunia; hawa ‘millennials’ ni kundi la vijana waliozaliwa kati ya miaka ya mwanzo ya 80 mpaka miaka ya mwanzo ya 2000. Nikasema acha niswali, nile daku kisha nirudi kuandika kuhusu kizazi hiki, maisha, uongozi, mafanikio na changamoto zake. Nilidhani itakuwa ni makala ya kuvutia na kuamsha tafakuri tunduizi juu ya tulipo na tunapoelekea.

Tupo kwenye zama ambapo huwezi kukwepa teknolojia ya habari na mawasiliano. Biashara, maisha, siasa na uchumi wote kwa ujumla unategemea sana teknolojia hii. Watu wanatafuta soko la bidhaa zao kwenye mitandao, habari zinapatikana mubashara kadri zinavyotokea, tena bila hata kufika chumba cha habari, bila kuchujwa wala kuwekwa sawa kwa matumizi ya walaji. Tunalipia huduma kwa teknolojia ya dijitali, tunatembea na pesa kiganjani, hadi baadhi ya mitandao leo hii inatoa mikopo midogo midogo kiganjani tu.

Ukiitazama hali tuliyopo na kuchambua mazingira yetu ni lazima utakubaliana na mimi kwamba fikra tofauti zinahitajika kila eneo; biashara, siasa na maisha ya kila siku ya Jamii ni lazima vibadilike ili kuendana na mahitaji ya nyakati (adaptability); watu (wamiliki wa biashara, waendeshaji na wasimamizi wa sehemu za kazi, viongozi na watumiaji wa huduma) ni lazima tubadilike kuendana na nyakati; pia mifumo ya kufanyia kazi, kutunza kumbukumbu, kufanyia maamuzi, kutolea huduma ni lazima ibadilike kuendana na mahitaji ya nyakati, mikakati ya biashara, ya kisiasa na ya kijamii ni lazima pia ibadilike kuendana na nyakati.

Neno uhakika (certainty) kwenye biashara, kwenye siasa, kwenye maisha ya jamii ya kila siku linapotea kwenye zama hizi. Hakuna uhakika kwa sababu sayansi ya mawasiliano inakuja na vitu vipya kila kukicha, mahitaji ya soko ni mapya kila siku, wateja wanataka vitu vipya kila siku.

Tamaa ya kuja na vitu tofauti inaongezeka kila siku. Ubunifu kwenye zama za dijitali ni chakula cha kila siku. Hakuna kiongozi wa biashara ama taasisi yoyote ile kwenye zama hizi anaweza akajisifia ana uhakika na anachokifanya. Teknolojia inayobamba leo hakuna mwenye uhakika kama tukiamka kesho itakuwa inalipa ama la. Mabadiliko ya haraka ya teknolojia yanafanya uwanja wa biashara, soko, siasa na maisha ya kila siku ya jamii upoteze uhakika kabisa!

Biashara, maisha ya kila siku na uongozi katika zama hizi za dijitali, hata kidogo hautegemei kuwekeza zaidi kwenye kuwa na uhakika ama kwenye udhibiti wa miundo ya biashara, sababu mazingira ya zama hizi si ya uhakika, hivyo viongozi na waendeshaji wa biashara ama taasisi wanapaswa kuweka mazingira yanayoruhusu ubunifu, mabadiliko, ushirikiano, mshikamano, na wakati huo huo yanayotoa fursa ya kukidhi mahitaji ya mtu binafsi mmoja mmoja; mazingira haya yatasaidia oganaizesheni kuendana na kukosekana kwa uhakika kunakokuja na zama zenyewe.

Atakayewahi kushtukia mchezo huu kwa hakika atawashinda wenzake sababu miaka ya sasa kuwa wa kwanza (pioneer) ni kila kitu, kama lengo ni kuvuna mazao bora zaidi ya washindani wako. Mfano, aliyevamia mwanzoni teknolojia ya pesa ya kwenye simu za kiganjani (mobile money) lazima alipata wateja wengi na ataendelea kushika bendera ya mstari wa kwanza kwenye huduma hii kuliko walioiga.

Katika zama za dijitali, mfano, ni ajabu kukuta bado watumishi wanapelekana semina Bagamoyo, Kibaha ama Morogoro kwa ajili ya mafunzo ya wafundishaji (training of trainers) ama kuna ‘tools’ (zana za kufanyia kazi) za kutengeneza, badala ya kufikiria kuwa na material kwenye podcast (mfumo wa usikivu) na mtumishi akafanya maandalizi yale yale, na kuweka kwenye tovuti maelekezo yote ili kila anayehusika aweze kusikiliza kwa muda wake na kujifunza popote alipo (ikiwa ni kwenye daladala, kwenye mazoezi na hata wakati anatembea kwa miguu).

Ninaweza kuongea kwa uhakika kabisa kuwa watakaofanikiwa ni wale watakaokuwa tayari kubadilika haraka ili kuendana na nyakati na hata kidogo siyo wale wahafidhina na warasimu watakaojaribu kuukataa uhalisia wa mahitaji ya nyakati. Hivyo, viongozi wa taasisi (CEOs) watakaofanikiwa kwenye zama hizi ni wale watakaokuwa wabunifu (creative) na watakaokubali kuitika wito wa kuendana na mabadiliko ya nyakati haraka (readily adaptive leaders).

Pia, kiongozi atakayefanikiwa kwenye zama hizi za kukosa uhakika ni ambaye, kwa mfano, ataweka utaratibu wa namna nzuri ya kufikia watumishi wake, wateja wake wote na ambaye ataweka mikakati yenye kanuni rahisi (strategy as simple rules) za Kathleen Eisenhardt, Profesa wa Chuo Kikuu Cha Stanford, Marekani, na wala siyo mikakati ya muda mrefu inayobana uvumbuzi, ubunifu na fursa ya kufanya maamuzi kwa haraka bila vizuizi vingi vya kimuundo, na inayokataana na wito wa mahitaji ya nyakati.

Mfano:- Leo hii mtu mashuhuri kama Diamond Platnumz ana washabiki zaidi ya milioni 3.6 kwenye jukwaa moja tu la Instagram; Jokate Mwegelo, zaidi ya washabiki milioni 2.6. Hawa vijana ni watu wa mfano (role models) kwa watu wa marika yao; millennials wenzao wanawaiga kuanzia kuvaa kwao, kula kwao, mtindo wa maisha yao, kila kitu! Huyu hahitaji gazeti kujitangaza ama kutangaza biashara yake.

Soko alilonalo linamtosha. Kuna millennials hawavushi siku lazima wapite kwenye ukurasa wake kuona leo kafanya nini! Ikiwa kuna kampeni ya siasa, watu watatazama anashabikia mgombea gani ama chama gani. Ama kama ni bidhaa ama fasheni akaisifia/akaianzisha kila mtu katika wafuasi wake atajua na kuna uwezekano wengi wakafuata. Mtu mmoja wa aina hii ana nguvu kubwa sana ya ushawishi kwenye jamii ya sasa sababu ya madhara aliyonayo kwenye jamii kupitia teknolojia mpya ya habari na mawasiliano.

Uongozi wa zama hizi lazima ujue namna ya kufanya kazi na watu wa aina hii. Biashara za sasa na taasisi mbali mbali lazima zijue nafasi ya teknolojia hii ili zijue mwitikio sahihi ni upi ili kukwepa kuachwa nyuma na wakati. Mwitikio (response) ambao nadhani utatusaidia kushinda mapambano katika zama za dijitali unapaswa uongozwe na utambuzi wetu wa mahitaji ya nyakati na ni lazima uyalenge makundi yote kwenye jamii sambamba na mahitaji hayo. Zama hizi ni lazima ziongozwe na viongozi wenye utayari wa kufanya majaribio (experimentation) na wenye uwezo wa kufanya maamuzi katika mazingira ya utata bila kusuasua.

Mazingira ya kazi, biashara, siasa na maisha ya jamii katika zama ambazo kizazi cha dijitali kinaingia kwenye soko la ajira kama waajiriwa na pia kwenye uchumi mpana kama wateja, ni lazima yazingatie mahitaji na uwezo wa kizazi hiki. Mfano: uwezo wao wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja (multi-tasking), mahitaji ya binafsi ya mtu mmoja mmoja (personalized needs) lakini wakati huo huo mahitaji ya kuwaunganisha pamoja watu mbali mbali, ambapo kuna ushirikiano kati ya watumishi ama wateja. Mwitikio ni lazima uweke uwezekano wa mabadiliko kufanyika kwa  urahisi (flexibility). Teknohama ikitumika ipasavyo ndiyo zana pekee ya kutuwezesha kuishi na kushindana ipasavyo kwenye zama hizi.

Leo kuwataka millennials wasome kitabu cha Shakespeare, ama Ngugi wa Thiong’o ama Shaaban Robert, lazima uwe utampa mtihani baadaye lakini siyo kwa kujifurahisha tu. Ila ukitaka uwafikishie hekima iliyojaa kwenye vitabu ama kwenye makala kama hizi, weka kwenye njia ya sauti ama kwenye mitandao ya kijamii unaweza ukawapata baadhi. Leo hii ukiandika kitabu weka pia nakala laini ya kimtandao (soft copy), na nakala ya sauti (podcast) ambayo msomaji anaweza ‘akasoma’ kwa kusikiliza kwa wakati wake (akiwa anaendesha gari, anafanya mazoezi ama anasafiri), vinginevyo utasoma mwenyewe kitabu chako!

Leo hii si lazima kwa mfano kumtaka mtumishi afike kazini saa moja na nusu asubuhi na atoke saa tisa na nusu kwa siku tano za kazi ndani ya wiki moja. Kama kiongozi unaweza kuishi na nyakati hizi, unaweza ukajaribu kuweka malengo ya kazi na namna ya kupima kama yamefikiwa na kutoa fursa kwamba mtumishi anaweza kuchagua siku moja ama mbili kwa wiki za kufanyia kazi nyumbani; ama akachagua masaa ya kuingia ofisini na kutoka kutegemeana na idara anayofanyia kazi.

Picha moja ya wakati wa kampeni inaweza kuwafikia wapiga kura hadi 1,000,000 ndani ya sekunde chache sana. Mazingira ya sekunde picha inaingia kwenye mtandao ni tofauti sana na dakika 60 baadaye. Hakuna uhakika kampeni ya Sasa hivi itakuwaje dakika 60 zijazo. Kwa hivyo tunakoelekea muundo wa kampeni hauwezi kuwa wa mikutano ya hadhara pekee. Kuna zana mpya zitaibuka na zitaamua nani ashinde.

Leo hii Tanzania tuna watu zaidi ya milioni 40 wenye simu za mikononi, gharama za data nazo zinashuka kila siku kutokana na uwepo wa mkongo wa Taifa, pia simu zenye mtandao wa mawasiliano zinashuka bei kwa kasi na kila mtu sasa hataki kubaki nyuma, ananunua na anatumia huduma za data. Kwa hakika uwanja wa mapambano unabadilika kila dakika.

Malezi na maadili ya Taifa ya leo ni tofauti sana na ya miaka 10 tu iliyopita na yatakuwa tofauti sana miaka 10 ijayo. Huwezi kujua mtoto uliyemzaa leo atakua kwenye zama zenye teknolojia ipi miaka 10 ijayo, na kwamba shule yake ya maadili itakuwa nini, na nani watakaoathiri zaidi mwenendo wa tabia zake.

Uhakika (certainty) ni neno lililofutika kabisa kwenye ulimwengu wa dijitali, utata (ambiguity) ni neno la uhakika zaidi kwenye zama hizi. Linatawala. Washindi wa zama hizi ni watakaoweza kuishi kwa kuendana na nyakati, baada ya kusoma mazingira na kuyaelewa, na pia, ushindi utakuwa na wale  walio wabunifu na wenye uwezo wa kubadilika haraka kadri teknolojia inavyoelekeza.

Namaliza makala yangu nikisema kwamba, siijui kesho ya Tanzania yangu, ya Afrika yangu, wala ya Jamii yangu. Hakuna lenye uhakika sana. Utata umetamalaki. Tunasukuma siku tu. Japokuwa ninaamini kufuata ‘strategy as simple rules’ ya Kathleen Eisenhardt hakutotuangusha; na ni lazima tuwe tayari kuyapokea mabadiliko na kufanya majaribio kila wakati. Pia ninaamini kwamba kuwa mbunifu na mwenye kwenda na nyakati ni mbinu zitakazotukwamua na changamoto ya mabadiliko ya haraka ya teknolojia.-—————————-

Dkt. Kigwangalla ni Mwanafalsafa aliyegeuka kuwa Daktari, Mjasiriamali, Mwanasiasa na Mtunga Sera.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here