Rais Dk. Magufuli ahutubia wananchi wa Msamvu Morogoro na Tegeta Dar akitokea Dodoma

0
83

Rais wa Jamuhuri Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli ameweza kuwahutubia wananchi mbalimbali waliojitokeza barabarani eneo la Stendi ya Mabasi Msamvu  Mkoani Morogoro wakati akitokea Mkoani Dodoma mapema leo  Julai 27,2017.

Katika tukio hilo umati  mkubwa uliofurika waliweza kumsikiliza Rais Dk. Magufuli na huku akipokea kero zao mbalimbali.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Manispaa ya Morogoro na viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuwaacha wafanyabiashara ndogondogo wa Mji huo waendelee kufanya biashara zao katika eneo la kituo cha mabasi cha Msamvu.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 27 Julai, 2017 baada ya msafara wake uliokuwa ukitoka Dodoma kuelekea Jijini Dar es Salaam kusimamishwa na wananchi wa Morogoro katika eneo la Msamvu na kumueleza kero ya kunyanyaswa na Manispaa ambao wamekuwa wakiwafukuza katika maeneo wanayofanyia biashara hasa baada kituo cha mabasi cha Msamvu kujengwa upya.

Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro SACP – Ulrich Onesphory Matei kuhakikisha Askari Mgambo hawawasumbui wafanyabiashara ndogondogo na amewataka wafanyabiashara hao kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri unaandaliwa kwa ajili yao.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewataka watu wote waliobinafsishiwa viwanda mbalimbali katika mkoa wa Morogoro kuvirejesha Serikalini endapo wameshindwa kuviendeleza ili wapewe wawekezaji wanaoweza kuviendeleza na kuzalisha ajira.

“Ninarudia wito wangu niliokwisha kuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha, na leo nataja akiwemo Mbunge wa hapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), narudia akiwemo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Pia Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wakulima wa mazao Mkoani Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na amewataja wakulima wa Wilaya ya Kilosa kwa kuongeza uzalishaji kutoka asilimia 42 msimu uliopita hadi kufikia asilimia 82 katika msimu huu.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi wa Morogoro kujitokeza kupata ajira wakati wa ujenzi, lakini amewataka  waliojenga katika hifadhi ya reli kuondoa majengo yao kwa hiari.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Morogoro

27 Julai, 2017 

Sehemu ya wananchi wa eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es salaam, wakimshangilia Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliposimama kuzungumza nao, alipokuwa safarini akirejea jijini Dar es salaam kutokea Mkoani Dodoma, Julai 27, 2017

Sehemu ya wananchi wa eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es salaam, wakimsikiliza Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliposimama kuzungumza nao, alipokuwa safarini akirejea jijini Dar es salaam kutokea Mkoani Dodoma, Julai 27, 2017

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na wananchi wa eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es salaam, baada ya wananchi hao kusimamisha msafara wake alipokuwa safarini akirejea jijini Dar es salaam kutokea Mkoani Dodoma, Julai 27, 2017.

Rais wa Jamuhuri Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli Akihutubia  Wananchi wa eneo la Stendi ya Mabasi Msamvu  Mkoani Morogoro waliokuwa wamejitokeza kumsalimia  akitokea Mkoani Dodoma. Julai 27,2017.

Rais wa Jamuhuri Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli Akimsikiliza Bi Maria Gabrieli aliyemweleza Mh Rais Juuu ya kero za wafanyabiasahara ndogondogo wa Stendi ya Mabasi Msamvu  Mkoani Morogoro kunyanyaswa. Julai 27,2917.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here