Kumekucha Sauti za Busara 2018, Jopo kukaa kuchuja maombi ya vikundi shiriki

0
187

Zaidi ya vikundi 400 vimeweza  kuwasilisha maombi ya ushiriki wa Tamasha la 15 la Sauti za Busara ambalo litafanyika Mji Mkongwe , Zanzibar kuanzia tarehe 8-11 Februari 2018.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya tamasha hilo imebainisha kuwa, zoezi hilo la maombi tayari limeshafungwa kuanzia 31 Julai,2017  ambapo ndani ya mwezi huu wa Agosti,  jopo la uteuzi linatarajia kukaa na kuchagua vikundi hivyo.

Imebainishwa kuwa, maombi yote hayo yatakayopatikana kabla ya tarehe ya mwisho, vikundi 40 vitachaguliwa kushiriki kwenye tamasha mwezi Februari 2018, kawaida vikundi takribani 20 vitaiwakilisha Tanzania na vinginevyo kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika na kwingineko.

Aidha, kwa upande wake Bi Marya Hamdan, kiongozi wa kikundi cha Tausi Women’sTaarab anasema “Sauti za Busara huleta faida kubwa sana kwa wasanii wa ndani na vilevile hata wapenzi wa muziki. Kwa miaka mingi sasa Sauti za Busara inatutangaza na kutufanya kuwa bora zaidi, kutupa sehemu ya kuonyesha kazi zetu na uwezo wetu. Tumejifunza mengi baada ya kukutana na wasanii mbalimbali kutoka nje ya Nchi wanaokuja kwenye tamasha. Vilevile tumejifunza mengi katika semina mbalimbali pamoja na kukutana na waandishi wa habari kutoka dunia nzima”.

 Kila mwaka wasanii mbalimbali hualikwa kufanya shoo katika matamasha barani Afrika, Ulaya na kwingineko baada ya kushiriki kwenye tamasha la Sauti za Busara. Mpaka sasa baadhi ya wasanii walioonekana baada ya kushiriki kwenye Sauti za Busara ni Msafiri Zawose, Jagwa Music, Leo Mkanyia, Jahazi Modern Taarab, Tausi Women’s Taarab, Culture Musical Club, Maulidi ya Homu ya Mtendeni na wengineo wengi. Kitu cha kupendeza ni kwamba wote hao wameonyesha muziki wa kweli na wenye asili ya Afrika ambao ni tunu na adimu kwa Afrika Mashariki.

 Sauti za Busara inaheshimu na kuthamini muziki wa Afrika Mashariki. Tamasha huonyesha thamani ya muziki wetu wa asili, pamoja na ajira na kipato wakipatacho. Tamasha huwavutia wageni kutoka sehemu mbalimbali za dunia na wengine huja kila mwaka. Mwezi wa februari sasa ni muda wa pilikapilika katika Nyanja za kitalii Zanzibar, tamasha lilipoanza mwaka 2004, februari ilikuwa ni mwezi wa kawaida sana ambapo wageni kama 3000 tu ndio waliokuwa wakitembelea Zanzibar lakini kwa sasa hali imebadilika ambapo wageni wamefikia 40,000.

 Sauti za Busara inaandaliwa na Busara Promotions, taasisi isiyo ya kibiashara (NGO) ambayo imesajiliwa Zanzibar. Dhima ya tamasha lijalo ni United in Music. Mpaka sasa Sauti za Busara meshaorodheshwa na BBC, CNN na jarida la Songline kama moja ya matamasha bora barani Afrika. Kwa sasa wanatafuta wadhamini na vyombo vya habari vya kushirikiana navyo ili kuhakikisha #SzB2018 ilivunja rekodi ya sasa.

Kwa taarifa zaidi: www.busaramusic.org

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here