Rais Magufuli ataka BOT idhibiti matumizi ya fedha za kigeni kwenye biashara na huduma nchini

0
141

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni katika biashara na huduma hapa nchini ili kulinda nguvu ya fedha ya Tanzania na kukabiliana na uhalifu wa kifedha.

Mhe. Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Desemba, 2017 wakati akifungua tawi la benki ya CRDB-LAPF Dodoma na kubainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka BOT kuongeza usimamizi wa benki zinazoendesha shughuli zake hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinajiunga na mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki na kufuatilia kwa ukaribu utendaji wake wa kila siku ili ziwe na manufaa kwa nchi.

Hivi sasa kuna benki 58 hapa Tanzania, BOT ni lazima mzifuatilie kwa ukaribu benki hizi, na zile zisizofanya vizuri chukueni hatua mara moja, ni bora tubakiwe na benki chache kuliko kuwa na benki nyingi zinazofanya vibaya”

“Pia nataka mdhibiti matumizi ya Dola, hivi navyozungumza kuna Dola Milioni 1 zimekamatwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini  m.caDar es Salaam, hakuna maelezo yoyote juu ya kuingia fedha hizo, ni lazima tuwe makini” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ameipongeza benki ya CRDB kwa kuendeshwa kwa ufanisi tangu ilipobinafsishwa kutoka Serikalini ambapo katika kipindi cha miaka 10 imelipa kodi serikalini kiasi cha Shilingi Bilioni 800, imetoa ajira kwa Watanzania 3,200, imetoa gawio Serikalini la Shilingi Bilioni 19.5 mwaka huu na imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.5 ambapo Shilingi Trilioni 1 kati yake zimeelekezwa katika sekta ya viwanda na kilimo.

Kuhusu kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali zitakazoongeza kasi hiyo zikiwemo kupunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana za benki za biashara kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu kutoka asilimi 10 hadi 8, kushusha riba ya Benki Kuu mara mbili kutoka asilimia 16 hadi 9, kutoa mikopo maalum kwa benki za biashara, pamoja na Benki Kuu kununua fedha za kigeni kwenye soko la jumla la benki ili kuongeza ukwasi wa shilingi kwenye uchumi.

“Kutokana na hatua hizi nimeambiwa kuwa hali ya ukwasi imeanza kuimarika na kusaidia kupunguza riba katika soko la fedha baina ya benki (IBCM rate) kutoka asilimia 13.69 Desemba 2016 hadi kufikia asilimia 3.29 Novemba 2017, pia riba katika soko la dhamana za Serikali zimepungua kutoka wastani wa asilimia 15.12 hadi 8.76 katika kipindi hicho” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa benki zote nchini kuanzisha matawi ya benki vijijini na kuwakopesha wajasiriamali ili waweze kuongeza uzalishaji hasa kilimo na viwanda, na pia ametaka wananchi wanaopata mikopo wazingatie kurejesha.

Mapema katika maelezo yake Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Dkt. Charles Kimei amempongeza Mhe. Raia Magufuli kwa juhudi kubwa za kuimarisha uchumi zikiwemo ujenzi wa viwanda, ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa barabara za juu (Flyover) na ameahidi kuwa CRDB yenye matawi 469 na wateja 3,500,000 ikiwa ndio benki inayoongoza kwa mtandao mkubwa nchini, itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha wajasiriamali na uwekezaji katika viwanda na kilimo.

Dkt. Charles Kimei na Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bw. Ally Laay wamekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 100 kwa Mhe. Rais Magufuli kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii, na Mhe. Rais Magufuli amekabidhi hundi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Satano Mahenge kwa ajili ya ujenzi wa wodi katika hospitali ya Mkoa Dodoma.

Ufunguzi wa tawi la CRDB LAPF Dodoma umehudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Samwel Malecela na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Isdor Mpango.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dodoma

13 Desemba, 2017

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here