Dk. Kigwangalla, hiyo wizara ina dhamana kubwa, usiichukulie poa!

0
138

Dk. Hamisi Kigwangalla, Mbunge wa Nzega Vijijini alipoteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii tarehe 7 Oktoba 2017 kutoka kuwa Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wachambuzi wengi wa mambo ya siasa na wa sekta ya maliasi waliona ametwikwa mzigo mzito katika kipindi muhimu ambapo Serikali ya Awamu ya Tano imejizatiti kupambana na ufisadi na ubadhirifu.

Sekta ya Maliasili ina mambo mengi na changamoto zake nyingi zinajulikana. Hakika Dk. Kigwangalla mwenyewe alionesha kutambua hilo alipowataka watanzania kuendelea kumuombea dua mara tu baada ya kupata taarifa za uteuzi wake kutekeleza majukumu yake mapya.

Lakini katika utendaji wake miezi hii michache ya wadhifa wake huu mpya, wachambuzi hawana budi kujiuliza kama dua tu za watanzania zinatosha na kama kweli Dk. Kigwangalla ametambua nini kiini halisi cha changamoto za Sekta ya Maliasili hadi kuifanya Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa kaa la moto hadi kufikia kufikia kuongozwa na mawaziri 13 ndani ya miaka 29.
Labda anafahamu kuwa sekta hii ina mapato makubwa sana kutoka rasilimali za maliasili na utalii hivyo kuwa na maslahi kwa watu wengi hasa wafanyabiashara na wanasiasa na hivyo kusababisha tuhuma zisizoisha kuhusu rushwa na ufisadi. Kashfa za uuzwaji wa pori la Loliondo, kuuzwa kwa hoteli za serikali kwa bei ya kutupa, uuzwaji wa vitalu na biashara haramu ya pembe za ndovu ni baadhi tu kwenye orodha ndefu ya yanayozungumziwa vibaya juu ya sekta hii.

Pia labda atakumbuka kashfa kubwa iliyotokana na Operesheni Uhai lililokuwa na lengo la kutukomeza vitendo vya ujangili na pia atakumbuka Anthony Diallo, aliyeshikilia wizara hiyo hapo awali aliwahi kusema kuwa hizara hiyo “imezungukwa na watu ambao wana mambo yao wanafanya” ikiwemo watendaji kumtengenezea majungu baada ya yeye kama waziri kuwabana kwenye biashara yao ya magogo.

Pia hapo awali tembo wengi sana waliuawa na uwindaji haramu ulishamiri huku watendaji wakionekana kutofanya yanayohitajika ili kukabiliana na tatizo. Kwa maani hiyo, waziri yeyote aingiapo Wizara ya Maliasili na Utalii akithubutu kupambana na rushwa na ufisadi, basi ajue anatengeneza maadui wa ndani wakishirikiana na wenye maslahi binafsi huko nje ya wizara.

Lakini kama kweli anayatambua haya na mengine mengi, mbona utendaji wake Dk. Kigwangalla unaonekana kama anataka kuingia kwenye mtego ambao waliomtangulia walifanya? Je, waziri huyu anategemea kupita njia ile ile waliyopita wenzake na kupata matokeo tofauti? Mara tu alipoanza majukumu yake mapya, alikutana na kazi ya wanamtandao wanaolinda maslahi ya wachache kwenye sekta ya maliasili iliyosambazwa mitandao ya kijamii:

“BREAKING NEWS
Mkakati mkali umeandaliwa na Waziri Kigwangalla, na timu yake ili kuzififisha taarifa zote za magazeti na televisheni juu ya kuwapo kwa makundi makubwa ya mifugo Loliondo.
Taarifa za uhakika ni kuwa Waziri ameshauriwa afike Loliondo haraka iwezekanavyo ili apate picha za kuonyesha hakuna mifugo. Yote hii ni katika kusafisha hali ya hewa kutokana na agizo lake batili la kuruhusu mifugo kuivuruga Loliondo na pia Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Waziri atakuwapo huko kwa siri kubwa, akiwa na timu ya waandishi hasa wapigapicha wa televisheni. Ziara hii atatumia magari mawili hivi. Zitapigwa picha mahali kusikokuwa na mifugo na kuwaaminisha wananchi kuwa Loliondo na Serengeti hakuna mifugo. Atataka kuonyesha kuwa waandishi ni waongo!

Usiku huu alitarajiwa kulala hoteli ya Acacia, Karatu, tayari kwa safari ya kesho Loliondo. Naambiwa tayari maandalizi yote yamekamilika hapo hotelini. Huu ndio ushauri aliopewa na washauri wake, Gambo, Nasha na wengine wa aina yao. Simameni imara kutetea uhifadhi.

Usiku mwema.”

Dk. Kigwangalla inambidi afikirie ‘nje ya boksi’ kama anataka kufanikiwa kuijenga Wizara hii kama dhamana aliyopewa na Mh. Rais. Alipopokea uteuzi huu alikuwa ana kati ya mawili: aidha ajiunge na mtandao wa ufisadi kwenye sekta ya maliasili au apambane na rushwa. Inavyoonekana, ameamua na kuchagua kupambana na vitendo viovu. Hivyo basi, hana budi kufanya tofauti na haya ni baadhi ya mikakati ambayo anaweza kuitumia:

1. La kwanza, afahamu fika hawa wanamtandao wabadhirifu katika sekta ya maliasili hawataacha kupambana naye eti kisa tu anakwenda na kasi ya mheshimiwa Rais ya kupambana na ufisadi na rushwa. Mtu akiwa anakula chake, ukitaka kumpokonya atapambana na yeye akishikilie kwa nguvu zote! Ndivyo wafanyavyo hawa ndugu zetu walio ndani ya wizara wakishirikiana na wafanyabiashara katika sekta hii.

Hivyo basi, lazima awaoneshe hawa kuwa vita hii ni endelevu na amewatambua kuwa wao ni vikwazo. Morali yake ndiyo itashusha morali ya wasiotakia sekta hii mema maana wao watafahamu fika kuwa si tu Mheshimiwa Rais yuko nyuma yake, bali taifa nzima.

2. Kuna haja ya kuonge faragha na Mheshimiwa Rais juu ya vikwazo hivi apewe rungu zaidi kusafisha hii wizara. Malengo yake, ya wizara yanaendana na yake ya Rais na agenda ya serikali ya awamu ya tano. Sababu moja kwa nini kuna watendaji wenye viburi ni kwa sababu kama wengi wao husema “sisi siku zote tupo Mawaziri huja na hutuacha hapa!” Muda umefika kuonesha kuwa sasa upo uwezekano mkubwa waziri akabaki n awatendaji wakaondolewa kama si waaminifu! Mtandao wa kifisadi kamwe hauwezi kuvunjwa kwa kuwepo na uwoga kuwa watendaji hawawezi kubadilishwa.

3. Kama ‘mashine ya mawasiliano’ ndani ya Wizara nayo imetekwa na wanamtandao hawa na ndiyo wanashirikiana na waandishi wa habari wasio wazalendo kutendeneza mizengwe na kupika majungu ili waziri aondolewe? Basi hakuna budi waziri huyu kuhakikisha ana kuwa na mbinu mbadala za kufikisha taarifa muhimu kwa wananchi hadi pale watendaji wanaomuhujumu watakapobainika na kushughulikiwa.

4. Waziri akaribishe maoni kutoka kwa walio chini ya utawala wa juu wa wizara ya jinsi waonavyo kinatakiwa kifanyike kurudisha siyo tu heshima ya wizara bali pia kuiweka sekta nzima ya maliasili na utalii katika hali ya kuaminika na kuwa shirikishi kama vili ilivyolengwa kwenye dira na dhima ya wizara.

Sambamba na haya, kuwe na mpango maalum wa kutambua kazi nzuri zinazofanywa na watendaji wa serikali ambao ni wachapakazi na waadilifu. Muda umefika sasa kurudisha utamaduni wa wale wanaofanya mema kuthaminiwa na wabadhirifu kuaddibiwa.

Kuna mengi zaidi Waziri anaweza kufanya ila kwa muda huu, haya ndiyo ya msingi. Akichelewa, yatamkuta ya mawaziri waliyopita.

Baadhi ya kurasa za mbele za magazeti zilizochapishwa juu ya Waziri Dk.Kigwangalla

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here