Rais Magufuli afungua barabara za Uyovu-Bwanga na Isaka – Ushirombo

0
366

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 10 Machi, 2018 amefungua barabara ya lami ya Uyovu – Bwanga Mkoani Geita na barabara ya lami ya Isaka – Ushirombo Mkoani Shinyanga na kuwataka Watanzania kutumia miundombinu hiyo kuongeza uzalishaji mali utakaosaidia kukuza kipato na kujenga uchumi wa nchi.

Akitoa taarifa katika sherehe za ufunguzi wa barabara ya Uyovu – Bwanga zilizofanyika Runzewe Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara hapa nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 45 na upana wa meta 11, umegharimu Shilingi Bilioni 47 na Milioni 917, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Katika sherehe za ufnguzi wa barabara ya Isaka – Ushirombo zilizofanyika katika
Mji wa Kahama, Mhandisi uMfugale amesema ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu
wa kilometa 132 umegharimu Shilingi Bilioni 193 na Milioni 897.

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Elias John Kwandikwa amesema kujengwa kwa barabara hizo ni muhimu kwa mawasiliano ya ukanda wa mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Shinyanga na Kigoma ambazo zinaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mhandisi Kwandikwa amebainisha kuwa miradi hiyo imetekelezwa sambamba na miradi mingine ya barabara za lami za Bwanga – Biharamulo (Km-67), Nyakanazi – Kakonko (Km-50), Ushirombo – Lusahunga (Km-110) na Kidahwe – Kasulu (Km- 63) na kwamba kwa sasa maandalizi yanafanywa ili kuanza ujenzi wa barabara nyingine za lami za Geita – Bulyanhulu (Km-58.3), Bulyanhulu – Kahama (Km-61.7), Nyamirembe – Katoke (Km-50) na usanifu wa barabara ya Ushirombo – Lulembera – Katoro (Km-56) na Lutembelumasa – Ipalamasa – Mbogwe – Masumbwe (Km-98).

Akizungumza na wananchi wa Runzewe Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi hiyo kwa gharama kubwa kutokana na hatua madhubuti inazochukua kujenga uchumi na amewataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha wanalinda amani iliyopo na kuchapa kazi.

Amewasihi wazazi na walezi kuwaeleza vijana wao juu ya athari za kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutatua kero za wananchi na kuwajengea mazingira bora ya kilimo, ufugaji na biashara ikiwemo kulifanyia kazi ombi la kuongezewa maeneo ya kilimo na ufugaji kutoka kwenye hifadhi kutokana na mahitaji yao kuongezeka.

Akiwa njiani Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Masumbwe katika Wilaya ya Mbogwe na kuwahakikishia kuwa ahadi yake ya kuwajengea kilometa 5 za barabara ya lami katika Mji huo itatekelezwa.

Akizungumza na wananchi wa Kahama kabla ya kufungua barabara ya Isaka –
Ushirombo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wakulima kwa namna walivyoitikia
wito wa kuongeza juhudi katika kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo Mpunga na
Pamba.

Mhe. Rais Magufuli ameagiza wananchi waliojenga makazi yao katika eneo la ekari 308 kati ya eneo lote la Mwamva lenye ekari 348 lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, wasiondolewe na kwamba eneo lililobaki la ekari 40 ndilo litumike kujenga chuo hicho na wananchi wasilivamie.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga kwa
uwakilishi mzuri wa wananchi wao na amewahakikishia kuwa maombi yao ambayo ni
kukomesha unyanyasaji dhidi ya wamachinga na wachimbaji wadogo wa madini,
kuongeza fedha katika hospitali na kupanua usambazaji wa maji katika maeneo
machache yaliyobaki yatafanyiwa kazi.

“Wabunge wenu wanashukuru kuwa sasa maeneo yao mengi yanapata maji safi na
salama, naomba wananchi mjipongeze wenyewe kwa kuwa hizo ni kodi zenu, na
Serikali ninayoiongoza itaendelea kuhakikisha wananchi mnapata mahitaji
mnayostahili, ninachowaomba tuilinde amani yetu na tuchape kazi” amesema Mhe.
Rais Magufuli.

Kesho tarehe 11 Machi, 2018 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake kwa
kufungua kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha Kahama Oil Mill kilichopo
Mkoani Shinyanga na Kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha Mount Meru
Millers Limited kilichopo Mkoani Singida.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kahama

10 Machi, 2018

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here