Rais Magufuli afungua viwanda Shinyanga na Singida

0
313

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara Fedha na Mipango kutatua vikwazo vinavyosababisha viwanda vya ndani vya kusindika mafuta ya mbegu zinazozalishwa hapa nchini kushindwa kushindana na mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi ikiwemo tozo za
kodi.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 11 Machi, 2018 katika sherehe za uzinduzi wa kiwanda cha kusindika mafuta ya kula Mjini Singida (Mount Meru Millers Ltd) baada ya kupokea taarifa ya mmiliki wa kiwanda hicho Bw. Atul Mittal aliyeiomba Serikali iondoe kodi ya ongezeko la thamani kwa mafuta ya mbegu zinazolimwa hapa nchini.

Bw. Atul Mittal ameongeza kuwa hatua hiyo itawezesha mafuta yanayozalishwa hapa nchi kumudu ushindani dhidi ya mafuta kutoka nje ya nchi na hivyo kuchochea uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta yakiwemo alizeti na pamba na kuongeza ajira kupitia kilimo na viwanda.

Pamoja na agizo hilo Mhe. Rais Magufuli pia ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuangalia namna nzuri ya kuwapunguzia kodi wafanyabiashara wanaowekeza viwanda hapa nchini na kuongeza viwango vya kodi kwa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi ili kuvilinda viwanda vya kusindika mafuta ya kula vya ndani.

“Mimi chama changu kimeniagiza nizalishe ajira, siwezi kutengeneza ajira za kwenye majukwaa, ni lazima kuwe na viwanda vya kuwajiri hawa watu.

“Kiwanda hiki kinazalisha tani 90,000 za mafuta kwa mwaka wakati uzalishaji wa nchi nzima ni tani 135,000, hii ni asilimia 30 tu ya mahitaji ya tani 450,000 na huenda yakaongezeka hadi kufikia tani 500,000 kwa mwaka kutokana na ongezeko la watu, ni dhahiri tunahitaji viwanda vingi kama hivi, lakini ili viwanda hivi viweze kuhimili ushindani tunahitaji kuvilinda dhidi ya viwanda vya nje, ndio maana nawaomba viongozi wenzangu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi na viongozi wengine tuhakikishe tunavilinda viwanda hivi kwa gharama zozote” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza mmiliki wa kiwanda cha Mount Meru Millers Bw. Atul Mittal kwa uwekezaji huo uliowezesha kupatikana kwa ajira za kudumu 300 na za muda 900 na ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi mapendekezo aliyoyatoa yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula hadi kutosheleza mahitaji kwa asilimia 100 katika kipindi cha muda mfupi ujao.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara kuacha kulalamika na badala yake kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo za pamba, dripu za maji ya wagonjwa, dawa za binadamu na viwanda vya kusindika mafuta ya kula badala ya kufanya ujanjaujanja wa kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi kwa madai kuwa ni ghafi wakati ni safi.
Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amezindua viwanda vya kampuni ya Kahama Oil Mills vinavyozalisha bidhaa za plastiki, chuma, mabati na mabomba ya maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kahama Oil Mills Bw. Mhoja Nkwabi Kabalo amesema viwanda hivyo vina uwezo wa kuzalisha bidhaa bora kwa ajili ya mahitaji ya ndani ya nchi na ameongeza kuwa hivi karibuni kampuni hiyo inatarajia kufungua viwanda vingine vinne ambavyo ni kiwanda cha kukamua alizeti tani 150 kwa siku huko Kibaigwa Dodoma, Kiwanda cha
kuzalisha mikate 4,000 kwa saa huko Miyungi Dodoma, Kiwanda cha Nyama kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata ng’ombe 70 na mbuzi 200 kwa saa huko Nyakakarango Mkoani Geita na kiwanda cha maji tiba Mkoani Shinyanga.

Pamoja na kumpongeza Bw. Mhoja Nkwabi kwa uwekezaji huo Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Serikali kuhakikisha wakandarasiwanaopata zabuni katika miradi ya Serikali wanatumia bidhaa
zinazozalishwa na viwanda vya ndani na amewataka wazalishaji wa bidhaa
hizo kuzalisha bidhaa bora.
Akiwa njiani kutoka Kahama Mkoani Shinyanga kuelekea Singida Mhe.
Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Tinde na Igunga na
kuwahakikishia kuwa Serikali itatekeleza ahadi ilizozitoa na amewataka
kuchapa kazi na kulinda amani.
Mhe. Rais Magufuli amewasili katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
11 Machi, 2018

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here