KIGWANGALLA AFUNGUA MAONESHO YA KIMATAIFA YA UTALII YA KARIBU/KILI FAIR 2018

0
114

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ametoa wito kwa taasisi za Serikali, jamii, sekta binafsi na wadau kwa pamoja kushirikiana kuendeleza utalii katika maeneo yao ili sekta hiyo iweze kunufaisha zaidi taifa kwa kiwango kinachostahiki kuliko ilivyo hivi sasa.

 

Ametoa wito huo juzi katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi wakati akifungua maonesho ya kimataifa ya utalii ya Karibu/Kili Fair 2018 ambayo yameshirikisha makampuni na wadau wa utalii zaidi ya 350 kutoka nchi zaidi ya 12 duniani huku na kuvutia watu zaidi ya 4,000 kuyatembelea.

 

Amesema ushirikiano huo utaiwezesha sekta hiyo kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa ambao kwa sasa ni takriban asilimia 17.2 ya pato la Taifa, zaidi ya asilimia 24 ya mapato yote ya fedha za kigeni sambamba na zaidi ya asilimia 10 ya ajira zote nchini.

Amesema mchango huo bado ni mdogo ukilinganisha na aina na idadi ya vivutio vilivyopo hapa nchini.

Dkt. Kigwangalla amesema Serikali ya awamu ya tano imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali zitakazosaidia kuboresha sekta hiyo ikiwemo ujenzi unaoendelea wa reli ya kisasa ya Standard Gauge, ujenzi wa Terminal 3 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Saalam na uboreshaji wa Shirika la Ndege la ATCL.

Pamoja na hayo amesema Serikali kupitia wizara yake inaendelea na mpango wa kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ambapo Mapori matano ya Akiba mkoani Kagera na Geita yatapandishwa hadhi kuwa Hifadhi za Taifa (Burigi, Biharamulo, Kimisi, Ibanda na Rumanyika).

“Napenda kumshukuru sana Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuridhia mapendekezo yetu ya kupandisha hadhi Mapori matano ya Akiba kuwa Hifadhi ya Taifa ambayo itaitwa Chato National Park, ‘Tunatake pia advantage’ ya uwepo wa uwanja wa ndege wa Chato ambao unajengwa katika kiwango cha kutua ndege kubwa zitakazowawezesha watalii kufika katika hifadhi hiyo” amesema Dkt. Kigwangalla.

Amesema hatua hiyo itafungua utalii wa kanda ya Kaskazini Magharibi tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo ni kanda ya kaskazini pekee inayofanya vizuri zaidi kwenye sekta hiyo. Amesema mpango huo unakwenda sambamba na kufungua utalii wa kanda ya kusini ambapo mradi wa Kusimamia Maliasili na Kuendeleza Utalii Kanda ya Kusini (REGROW) upo katika hatua ya utekelezaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania, Devotha Mdachi amesema Serikali kupitia bodi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau kutangaza utalii wa Tanzania katika maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi sambamba na kuwashirikisha kunadi kauli mbiu mpya ya utalii wa Tanzania, “Unforgettable, Tanzania”.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye amesema kamati hiyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali na wadau hususan katika eneo la mabadiliko na maboresho ya sheria za kusimamia sekta hiyo iweze kuondokana na changamoto zilizopo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here