Uhakika wa amani, ulinzi na usalama ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha wananchi kuishi na kuendelea na shughuli zao za maendeleo.
Katika kuzingatia hilo, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) imeendelea kushirikiana na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa katika operesheni za ulinzi wa amani.
Akizungumza leo Mei 24, 2023 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Jujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024 alisema “JWTZ imeendelea kuwa na vikosi vya ulinzi wa amani katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika ya Kati na Lebanon chini ya Misheni za Umoja wa Mataifa na inashiriki katika Operesheni ya kupambana na ugaidi nchini Msumbiji”.
Aidha, Jeshi hilo lina maafisa wanadhimu kwenye operesheni za ulinzi wa amani nchini Sudan Kusini, Lebanon, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Vilevile, Mhe. Bashungwa alisisitiza “Ushiriki wa JWTZ katika operesheni za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa umeiwezesha nchi yetu kutimiza matakwa ya Umoja wa Mataifa na Jumuiya za Kikanda ya kushiriki katika ulinzi wa amani, kimataifa na kikanda. Pia, ushiriki huu unaendeleza Diplomasia ya Kijeshi, na unasaidia JWTZ kuongeza uwezo kwa kufanya kazi na nchi nyingine.