Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akifungua kikao kazi cha Maafisa Waandamizi wa Taasisi za Umma na Vyama vya Kitaaluma kilicholenga kujadili matumizi na uendeshaji wa mifumo ya kidigitali kilichofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewataka Wakuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Taasisi za Umma kushughulikia kwa wakati malalamiko na maoni ya Wananchi kupitia mifumo ya kidigitali ya e-mrejesho na e-uhamisho ili kuleta tija iliyokusudiwa.
Bw. Mkomi ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Waandamizi wa Taasisi za Umma na Vyama vya Kitaaluma kilicholenga kujadili matumizi na uendeshaji wa mifumo ya kidigitali kilichofanyika jijini Dodoma.
Sehemu ya Maafisa Waandamizi wa Taasisi za Umma na Vyama vya Kitaaluma wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi wakati akifungua kikao kazi kilicholenga kujadili matumizi na uendeshaji wa mifumo ya kidigitali kilichofanyika jijini Dodoma.
Amesema licha ya kuundwa kwa mifumo hiyo kama hakutakuwa na uwajibikaji wa kufanyia kazi maoni na malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi hao kutakuwa hakuna maana ya kuwa na mifumo hiyo.
“Mtakapokuwa mnachelewa kujibu malalamiko ya wananchi, wananchi hao wataandika barua kwangu huku wakielekeza barua hiyo ionwe na Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ni Mkuu wa Watumishi wote pamoja na kwa Waziri Mkuu, hatutaki kufika huko jibuni kwa wakati,” Bw. Mkomi amesisitiza.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika, akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi kufungua kikao kazi cha kujadili matumizi na uendeshaji wa mifumo ya kidigitali kilichofanyika jijini Dodoma
Kufuatia hatua hiyo, Bw. Mkomi amesema anataka kuona Maafisa watakaochaguliwa kusimamia mifumo hiyo wanawajibika ipasavyo ikiwemo kuhakikisha malalamiko ya wananchi yanajibiwa kwa haraka huku akisisitiza suala la usiri.
Ameongeza kuwa endapo mfumo wa e-mrejesho utatumika ipasavyo utasaidia Taasisi za Serikali kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi kwani mrejesho ambao utakuwa ukitolewa utasaidia katika kufanya maamuzi yanayoendana na hali halisi.
Amefafanua kuwa mfumo wa e-mrejesho umesanifiwa kwa namna ambayo unaongeza uwazi, uwajibikaji na usiri kwa kuwa ni mfumo unaowezesha viongozi kuona kwa jinsi gani malalamiko au maoni yanavyoshughulikiwa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akiwa katika kikao kazi cha kujadili matumizi na uendeshaji wa mifumo ya kidigitali kabla ya kufungua rasmi kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Dodoma.
Akizungumzia mfumo wa e-uhamisho, Katibu Mkuu Mkomi amesema, mfumo huo utakuwa wa wazi na utasaidia Watumishi kuomba nafasi ya kuhama au kuhamia mahali ambako kuna uhitaji wa watumishi na si vinginevyo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (Wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Waandamizi wa Taasisi za Umma na Vyama vya Kitaaluma baada ya kufungua kikao kazi cha kujadili masuala ya utawala bora kilichofanyika jijini Dodoma.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bi. Leila Mavika amesema kutumika kwa mfumo wa e-mrejesho kutasaidia Serikali kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi.
Aidha ameongeza kuwa taarifa mbalimbali zitakazopatikana katika mifumo hiyo itasaidia kuongeza utendaji kazi Serikalini.