KITAIFA

SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 45.5 KUTOKA KWA NMB

SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 45.5 KUTOKA KWA NMB

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea mfano wa Hundi ya Shilingi Bilioni 45.5 (Gawio la Serikali) kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Benki ya NMB yaliyofanyika Mlimani City Jijini Dar es Salaamtarehe 17 Juni, 2023. Wengine katika picha ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB Dkt. Edwin Mhede pamoja na Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu wakishuhudia.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameyataka
mashirika yote ya umma kujiendesha kwa ufanisi, tija na ushindani ili yaweze kuwa
endelevu.
Rais Samia ametoa tamko hilo leo wakati wa hafla ya benki ya NMB ya kukabidhi
gawio kwa Serikali na kusherehekea miaka 25 ya safari ya mafanikio ya benki hiyo,
iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kufanya tathmini ya utendaji wa
mashirika yote ya umma na yale ambayo Serikali ina hisa kubwa ili kubaini mashirika
yasiyo na faida yanayoshindwa kujiendesha na kuitia hasara Serikali.
Rais Samia pia amesema tathmini hiyo inafanywa na Msajili wa Hazina ambapo
Serikali itayachukulia hatua na kuyafuta mashirika ambayo hayafanyi vizuri,
kuyasaidia na kuyapa miongozo ya namna ya kujiendesha ili yapate faida.
Rais Samia amewataka wajasiriamali, wakulima na wananchi wote wanaohudumiwa
na benki ya NMB kuendelea kuwa waaminifu wanapochukua mikopo bila dhamana ili
benki hiyo iendelee kuwa na ustawi.
Benki ya NMB imekabidhi gawio la shilingi bilioni 45.5 ambapo Serikali inamiliki
31.8% ya hisa katika benki hiyo huku asilimia zingine zikiwa zinamilikiwa na wadau
kutoka sekta binafsi.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *