Baadhi ya Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata wakila kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kutunza siri kabla ya kuanza kwa mafunzo ya siku tatu yaliyoanza leo tarehe 19 Juni, 2023. Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Kata 14 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 13 Julai, 2023 kujaza nafasi wazi za madiwani.
Wasimamizi wa Uchaguzi wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua mafunzo ya Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata leo tarehe 19 Juni, 2023 jijini Tanga.
Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa kata 14 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 13 Julai, 2023 kujaza nafasi wazi za madiwani.
“Jambo muhimu mnalotakiwa kuzingatia ni kujiamini na kufanya kazi kwa weledi, mnapaswa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi mdogo,” amesema Jaji Mbarouk.
Amewaasa washiriki hao wa mafunzo kuhakikisha kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yao wanao katika uendeshaji wa uchaguzi, wahakikishe wanazingatia maelekezo watakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea.
“Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria ambazo hupaswa kufuatwa na kuzingatiwa, hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi,” amesema Jaji Mbarouk.
Amewataka watendaji hao wa uchaguzi kuvishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yao kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa ili kurahisisha utendaji wa kazi.
Jaji Mbarouk amewaelekeza wasimamizi hao wa uchaguzi kuhakikisha kuwa watendaji wa vituo vya kupigia kura ni watu wenye weledi na uwezo mkubwa na kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha vituo kufunguliwa saa 1:00 asubuhi siku ya kupiga kura.
Kata zilizotarajiwa kufanya uchaguzi mdogo ni pamoja na Ngoywa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Kalola iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Sindeni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Potwe iliyopo Halmashauri Manispaa ya Muheza, Kwashemshi iliyopo Halamshauri ya Wilaya ya Korogwe, Bosha iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Mahege iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na Bunamhala iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Nyingine ni, Njoro na Kalemawe zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mnavira iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Kinyika iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Magubike iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na Mbede iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.