Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (kulia)
akipewa taarifa ya utendaji kazi na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania na
Mtendaji Mkuu Nyakaho Mahemba (kushoto) Juni 20, 2023 jijini Dar es Salaam wakati
wa ziara ya kikazi katika wa Mfuko huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amewasisitiza watendaji na watumishi wa taasisi chini ya wizara hiyo kuwahudumia wadau wa sekta ya Utamaduni na Sanaa kwa wakati ili kuleta tija katika utendaji kazi.
Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema hayo Juni 20, 2023 jijini Dar es Slaaam alipofanya ziara ya kikazi katika taasisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Tanzania pamoja na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (katikati)
alipotembelea ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wakati wa ziara ya
kikazi katika katika taasisi hiyo Juni 20, 2023 jijini Dar es Salaam.
“Tuongeze ubunifu zaidi na kurasimisha wafanyabiashara wa kazi za Utamaduni na Sanaa na wasanii ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika utoaji wa huduma kwa wadau wa sekta zetu hizi” amesema Bw. Yakubu.
Ameongeza kuwa taasisi zote za Wizara zina wajibu kutekeleza vipaumbele vya Serikali ikiwemo kuongeza wigo wa wasanii kwenda kufanya kazi za Sanaa nje ya nchi na kutangaza Utamaduni na Sanaa ya Tanzania na kuongeza ubunifu katika utendaji kazi wao.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Tanzania Dkt. Kilonzo
Kiagho (katikati) akisisitiza jambo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na
Michezo Bw. Saidi Yakubu (wa kwanza kulia) alipofanya ziara ya kikazi katika taasisi
hiyo Juni 20, 2023 jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wao Katibu Mtendaji wa BASATA Dkt. Kedmon Mapana, Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Tanzania Dkt. Kilonzo Kiagho pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania Nyakaho Mahemba wamesema taasisi zao zitatekeleza kwa vitendo maelekezo ya Serikali ili kuwahudumia wadau wao.