KITAIFA

PROF. MBARAWA: BARABARA YA MNIVATA- NEWALA-MASASI NI KIUNGO MUHIMU

PROF. MBARAWA: BARABARA YA MNIVATA- NEWALA-MASASI NI KIUNGO MUHIMU

Serikali imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara kutoka Mtwara hadi Mnivata yenye urefu wa km 50, kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank-AfDB) na kufanikisha azma ya Serikali kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa sehemu iliyobaki ya kutoka Mnivata hadi Masasi.

Akihutubia Juni 21, 2023 katika hafla ya utiaji saini wa muendelezo wa ujenzi wa barabara hiyo, Mnivata – Newala – Masasi (km 160) pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa lengo ni kuwaondolea wananchi kero ya usafiri wa barabarani na kuboresha mtandao wa barabara na madaraja ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji, hivyo kukuza uchumi wa nchi yetu.

“Ujenzi wa barabara hii utakapokamilika utasaidia kuondoa adha ya usafirishaji wa mizigo na abiria na kuongeza usalama kwa wote watakaotumia barabara pamoja na daraja hili na itasaidia kukuza biashara mbalimbali. Vilevile itasaidia katika kufanikisha shughuli za kijamii kwa ujumla na itatoa mchango mkubwa katika shughuli za utalii. Pia, itaunganisha na kuboresha hali ya usafiri na usafirishaji wa malighafi za viwandani kama makaa ya mawe na cement, mazao ya chakula na kilimo, mifugo, uvuvi, bidhaa za kibiashara na mazao ya misitu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mtwara pamoja na mikoa jirani ya Lindi, Ruvuma na Pwani kwenda maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” alisema.

Aidha Waziri Mbarawa amesema kuwa, barabara hiyo pia ni kiungo muhimu kwa barabara kuu ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay inayojulikana kama Ushoroba wa Mtwara (Mtwara corridor) ambayo inaunganisha na nchi jirani ya Msumbiji. “Pamoja na manufaa makubwa niliyoyasema, pia inatarajiwa kwamba shughuli za kiuchumi za wananchi waishio maeneo mradi huu zitaimarika kwani mradi huu utasaidia kutengeneza ajira kwa wananchi wetu wakati wa ujenzi,”.

Alisema kuwa leo wameshuhudia utiaji saini wa Mikataba miwili. Mkataba wa Sehemu ya kutoka Mnivata hadi Mitesa yenye urefu wa Km 100 ambao utatekelezwa na Kampuni ya China Wu Yi Co. Ltd kwa gharama ya Shilingi Bilioni 141.964 na mkataba wa sehemu ya pili kutoka Mitesa hadi Masasi yenye urefu wa km 60 pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti ambao utatekelezwa na Kampuni ya China Communications Construction Co. Ltd kwa gharama ya Shilingi Bilioni 92.548. Hivyo, Mikataba yote miwili inagharimu jumla ya Shilingi Bilioni 234.512.

“Gharama ya ujenzi wa miradi hii miwili ni kubwa hivyo naomba tuzingatie thamani ya fedha ya mradi (Value for Money) wakati wa ujenzi. Naiagiza TANROADS kusimamia miradi hii kwa udhibiti mkubwa ili barabara pamoja na daraja la Mwiti viweze kutumika kwa muda uliopangwa (Design Life)” amesema.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Tanroards, Mha. Mohamed Besta amesema kuwa, Serikali ya Tanzania imepata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank (AfDB) kwa ajili ya mradi ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mnivata – Newala – Masasi (km 160) pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti.
“Ujenzi wa barabara hii ni moja ya miradi mingi ya barabara ambayo imetekelezwa kwa kugharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na Serikali,” amesema.

Aidha Besta amesema kuwa mradi wa Ujenzi wa barabara ya Mnivata-Newala- Masasi (km 160) pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti ni moja ya mikakati ya serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Mtwara hususani katika wilaya za Tandahimba, Newala na Masasi kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

“Kupitia mradi huu pia kutakua na miradi jumuishi kwa ajili ya kusaidia jamii katika wilaya zinazopitiwa na barabara hii. Hivyo, miradi ifuatayo itatekelezwa: Ujenzi wa shule, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia korosho, ununuzi wa magari ya wagonjwa na ununuzi wa X-rays.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *