Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali (TAMISEMI), Mhe.
Deogratius Ndejembi (Mb) amewaagiza Maafisa Elimu wa Mikoa na
Maafisa Elimu wa Sekondari wa Halmashauri nchini kuhakikisha
wanasimamia ujenzi wa miradi ya elimu usiku na mchana ili ikamililike
ifakapo Agosti 2023 na kuwawezesha wanafunzi wa kidato cha Tano
kupata miundombinu bora ya elimu.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo mkoani Tabora wakati
akifungua Kikao kazi cha Maafisa Elimu wa Mikoa na Maafisa Elimu wa
Halmashauri cha Tathmini ya Utekelezaji wa shughuli za elimu kwa mwaka
2022/23.
Amesema Serikali kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)
imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 7.5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, vyumba
vya madarasa na Matundu ya vyoo katika Shule za Sekondari za Kidato
cha Tano na Sita.
“Tumtie nguvu Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo usiku na mchana na kuhakikisha
inakamilika ili wanafunzi wa kidato cha tano watakaoripoti shuleni wawe na
miundombinu ya kutosha kulingana na idadi yao” Mhe. Ndejembi
amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI haitamfumbia macho
yeyote atakashindwa kusimamia na kukamilisha miradi hiyo ifikapo mwezi
Agosti 2023, kwani atakuwa ameshindwa kutekeleza wajibu wake
kikamilifu.
Aidha, Ndejembi amesema Serikali kupitia mradi wa SEQUIP imetoa
shilingi bilioni 21.18 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule
mpya 212 za Sekondari za Kata pamoja na Shilingi Bilioni 48 kujenga
Shule za Wasichana za Bweni za Mikoa katika mikoa 16.
Sanjari na hilo, amewataka Maafisa Elimu kufuata taratibu zilizobainishwa
katika kusimamia shughuli zote za Elimu ipasavyo ikiwemo ujenzi wa shule
mpya na miundombinu inayojengwa katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt.
Charles Msonde amesema katika Kikao kazi hicho watajadili kwa kina
kuhusu namna bora ya usimamimizi na Utekelezaji wa miradi elimu katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ikamilike na kuleta tija kwa wananchi na
maendeleo ya taifa.