NA GEORGE ALPHONCE – MWANA HABARI
Mbunge wa Kawe, Dar es Salaam Askofu Josephat Gwajima ameipongeza Serikali kwa kupelekea huduma ya usafi wa haraka (Mwendokasi) katika jimbo lake ambapo utiaji saidi wa ujenzi wa barabara zake umefanyika leo Juni 30, 2023 na kutaja awamu ya kwanza ya mradi huo itakuwa ni ujenzi wa kipande cha kutoka Mwenge hadi Ubungo ukigharamiwa kupitia program ya Dar es salaam Urban Transport Project (DUTP).
Akiongea katika hafla hiyo ya utiaji saini Gwajima amesema yeye kama Mbunge wa Kawe kipande kinachomuhusu sana ni kuanzia Mwenge, kuelekea Makongo jeshini, Lugalo, Mbezi beach, Tegeta mpaka Basiaya Kata ya Bunju na kwamba hizo ni habari njema kwasababu itasaidia sana wananchi kusafiri kwa kasi na kuokoa fedha zinazopotea kwasababu ya kuchelewa kwenye foleni.
“Nampongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa bidii yake kubwa kwenye kuitafuta fedha hii na kuona ni vyema kwamba atupe kipaumbele watu wa Kawe ili na sisi tupate mwendokasi kama ilivyo kwa watu wa Ubungo kwa ndugu yangu Kitila Mkumbo,”.
Aidha Gwajima alionesha kutokuridhika kwake na jinsi Serikali inavyotatua kero ya mafuriko kwa wakazi wa Basiaya, Nyamachabezi, Naishozi na Tegeta kwakuwa pia kwenye mpango huo wa ujenzi wa Barabara ya mwendokasi haupo kama alivyoahidiwa.
“Pia nioneshe kutokuridhika kwangu kama mwakilishi wa wananchi, kwa takribani miezi sita mmekuwa mkituambia kwamba ujenzi wa barabara ya mwendokasi kutoka Tegeta mpaka Basiaya utajumuisha mitaro ya maji ambayo itasaidia kuondoa mafuriko yanasombua watu wa Basiaya, Nyamachabezi, Naishozi na Tegeta kwa muda wa miaka 20 sasa.
“Nilipouliza Bungeni Waziri ukanijibu tutasaini leo tarehe 30 Juni 2023, kweli leo tunasaini lakini nilipofika hapa na kuangalia kwenye mpango kazi wa mradi huu ujenzi wa mitaro hiyo haumo, imekuwa ni siku ya huzuni kuliko zote kwasababu tulipopata taarifa kwamba itakuwepo tuliwahubiria wananchi, tumewaambia sasa tatizo la mafuriko limekwisha, kwasababu ni ahadi ya Mhe. Rais fanyeni kila linalowezekana, mfikirie na mlifanyie kazi ili mtusaidia sisi kama wawakilishi wa wananchi,” alisema Gwajima.