WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inataka kuona wananchi wakipatiwa huduma za afya huko waliko bila kulazimika kuzifuata mbali.
“Tumejenga vituo vya afya, hospitali za wilaya na sasa tunajenga hospitali kwenye kila Halmashauri ili kusogeza huduma zaidi kwa wananchi. Nia ya Serikali ya awamu ya sita ni kuona wananchi wetu wanapata huduma muhimu hukohuko waliko,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Julai 07, 2023) mara baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu na vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula zilizopo mkoani Mtwara.
Akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, Waziri Mkuu amesema kuwa malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuifanya hospitali hiyo iwe mkombozi kwa wana-Kusini na nchi jirani za Msumbiji na Comoro. “Anataka wananchi wasiende umbali mrefu kupata huduma, badala yake huduma zote ziishie hapo.”
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Afya kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na vifaa tiba vya kisasa kwenye maeneo yote ya utoaji wa huduma za afya. “Hospitali hii imetengewa shilingi bilioni tatu za kuboresha miundombinu na vifaa tiba.”
Amesema kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, Mtwara itaendelea kupata huduma mpaka pale itakapokamilika ili malengo ya ujenzi wa hospitali hiyo yaweze kutimia.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Radiolojia Mkuu, Dkt. Dennis Mosha alisema hospitali hiyo imefanikiwa kusimika Mfumo wa Matibabu (eMedical HMIS) kwa ajili ya uhifadhi wa taarifa za matibabu. “Hospitali inatumia mfumo wa utunzaji wa picha za X- Ray, CT SCAN na MRI katika kuhakikisha utoaji bora wa huduma kwa njia ya kidijitali. Tunaweza kuwasiliana na MOI ili kupata ushauri zaidi wa kitaalamu endapo tunakwama,” alisema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la ujenzi katika Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula na kusema lengo la Serikali ni kuona majengo hayo yanakamilika na hospitali inaanza kutoa huduma mara moja.
“Hatuhitaji kuona awamu za ujenzi zikichukua muda mrefu. Tunataka ujenzi uendelee ili ukamilike kwa haraka kwa sababu fedha zake zipo. Hakikisheni mkandarasi anamaliza jengo lote,” amesisitiza.
Muonekano wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Lobikieli Kisambu alisema jengo hilo la ghorofa moja, litakapokamilika litakuwa limegharimu sh. bilioni 4.68 na kwamba hadi sasa zimekwishatumika sh. bilioni 2.9. “Jengo la chini (ground floor) limekamilika kwa asilimia 88.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekagua mradi wa uboreshaji wa upatikanaji maji safi na salama katika chujio la maji lililopo Mangamba, linalosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA).
Ameitaka RUWASA na Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira nchini zifanye tafiti kwenye maeneo ambayo yanaweza kupatikana maji. “Jukumu hili si lenu peke yenu, shirikianeni na viongozi wa Halmashauri kuvibainisha na kuvilinda vyanzo hivyo ili dhamira ya Rais Dkt. Samia ya kupeleka huduma za maji safi hadi kwenye vitongoji iweze kutimia.”
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake mkoani mkoani Mtwara ambako jioni hii atazungumza na wakazi wa Manispaa ya Mtwara.