KITAIFA

WAZIRI DKT. CHANA ATOA MAELEKEZO MAHUSUSI KUHUSU MFUKO WA UTAMADUNI

WAZIRI DKT. CHANA ATOA MAELEKEZO MAHUSUSI KUHUSU MFUKO WA UTAMADUNI

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo  Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa Taasisi za Fedha za CRDB na NBC pamoja na Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania kutekeleza Makubaliano yaliyofikiwa katika kusaidia wadau wa Utamaduni na Sanaa.

Mhe. Chana ametoa wito huo Julai 8, 2023 Jijini Dar es Salaam mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya utoaji mikopo kwa taasisi za fedha za CRDB na NBC  na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, ambapo amesema mfuko huo ulikua ukitoa mikopo moja kwa moja kwa walengwa waliokusudiwa pasipo kushirikisha taasisi za fedha, hivyo kupitia makubaliano hayo, taasisi  hizo mbili za fedha  zitashirikiana kwa pamoja katika utoaji wa huduma ya mikopo kwa Wadau sekta ya Utamaduni na Sanaa.

“Mfuko huu tangu uzinduliwe umekua na mafanikio kadhaa ambapo sisi kama Serikali tunajivunia, miongoni mwa mafanikio hayo ni kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.077 kwa miradi 45 ya Utamaduni na Sanaa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Iringa, Mwanza, Mara, Mbeya na Dodoma. Aidha uwezeshaji uliofanyika kupitia miradi hii umzezalisha ajira 21,579” amesema Dkt.Chana.

Amesema katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia imedhamiria kutoa  mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 20 pamoja na kuzalisha ajira sizizopungua 1,000,000.

Aidha, mikopo hiyo yenye masharti nafuu itasaidia kuwakwamua kiuchumi wasanii na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko huo Bw. Abdulmajid Nsekela  ametoa wito kwa wadau hao kukopa mara baada ya kuwa na wazo la biashara pamoja na wakumbuke kurejesha, huku Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara Benki ya NBC Bw. Elvis Ndunguru akieleza kuwa mikopo watakayotoa itakua na riba ya asilimia 9 kiwango ambacho ni cha chini katika soko.

Naye Afisa Mtendaji wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania Bi. Nyakaho Mahemba ameeleza kuwa ili mwombaji apate mkopo anatakiwa kuwa na sifa, ikiwemo kuwa raia wa Tanzania, awe anatekeleza kazi ya Utamaduni au Sanaa, awasilishe andiko la mradi linalobainisha malengo mahususi ya mkopo na mchanganuo wa namna atakavyorejesha mkopo husika pamoja na kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka Serikali ya Mtaa na kijiji mahali ambapo mradi unafanyika.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *