Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama na (Mb) Peramiho akizindua Mradi wa Umeme Vijijini katika Kijiji cha Litowa kata ya Parangu Halmashauri ya Wilaya ya Songea
Wananchi wameaswa kutumia nishati ya umeme kubuni shughuli za maendeleo, zitakazochangia ukuaji wa kipato, kwa kutumia fursa zilizopo serikalini za upatikanaji wa mikopo.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama na (Mb) Peramiho wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijini katika Kijiji cha Litowa kata ya Parangu Halmashauri ya Wilaya ya Songea leo tarehe 11/07/2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama na (Mb) Peramiho akisimika nguzo katika kitongoji cha Tangini katika Kijiji cha Litowa kata ya Parangu Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Amebainisha kwamba vijiji 16 ambavyo vilikuwa havijapata umeme vitapata nishati ya umeme, ikijumuisha vitongoji vyote 8 vya kijiji cha Litowa ifikapo mwezi Disemba mwaka huu 2023.
Aidha kuna vitongoji 15 ambavyo ni mradi Maalumu wa Mhe, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambavyo vitapata umeme, vitongoji vinavyobakia vimewekwa kwenye Mpango na vitasimamiwa na shirika la umeme TANESCO ili viweze kupata umeme.
Madiwani Mhe. Monica Tambala na Mhe. Filbeta wakifukia nguzo katika Kitongoji cha Tangini mara baada ya uzinduzi Mradi wa Umeme Vijijini katika Kijiji cha Litowa Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
“Nishati ya umeme ni Mwanga, nishati ya umeme ni uchumi, lazima tufikirie mipango ya uchumi inayoendana na fursa ya upatikanaji wa nishati umeme”, alisema Waziri Mhagama,
Aliendelea kusema kuwa wanawake na vijana kwa kupitia fursa za Miradi ya maendeleo inayohusisha kujiunga katika vikundi vya kiuchumi itawawezesha kukopa mashine za kisasa uzalishaji zitakazokuwa zinatumia nishati ya umeme.
Akizungumzia kuhusu elimu Waziri Mhagama alisema nishati ya umeme itasaidia kupandisha ubora wa elimu na kutoa wito kwa walimu kuendelea kusimamia maadili kwa watoto ili utandawazi usiharibu mila na desturi njema za watoto katika jamii.
“Unyanyasaji wa watoto umeongezeka sana nawaomba wazazi tuwe karibu na watoto, ili tuweze kutambua tabia na mienendo yao ya kila siku”alisisitiza.
Diwani wa kata ya Parangu Mhe. Astrida Nchimbi (kulia) akifungia nguzo katika Kitongoji cha Tangini mara baada ya uzinduzi Mradi wa Umeme Vijijini katika Kijiji cha Litowa Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Julian Ludovic amesema Mkandarasi aliyepewa kazi ya kusambaza umeme katika Jimbo la Peramiho Halmashauri ya Songea amefikia 54% na kasi yake ya ukamilishaji wa mradi ni nzuri.
Naye Mratibu wa Umeme wa REA Wilaya ya Songea Bwn. Victor Kelvin Mahije amesema Mkandarasi amefanikiwa kuwasha umeme vijiji 14 na vijiji vingine viko katika hatua tofauti katika hatua ya ukamilishaji mradi huo, ikiwa ni pamoja na usimikaji wa nguzo na utandazaji wa nyaya.