Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho akizungumza na Wananchi katika kijiji cha Nakawale alipotembelea kujionea miradi mbalimbali ya maendeleo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho ametoa rai kwa wawekezaji wa mbalimbali katika jimbo la Peramiho kuendelea Kufanya uwekezaji wenye tija kwa wananchi, kwa Halmashauri na kwa Taifa.
Hayo ameyasema wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Muhukuru katika ziara yake ya kutembelea Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Songea leo tarehe 12/07/2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho akizungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Songea Vijijini Ndg, Thomas Masolwa (Kushoto) wakati wa Mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nakawale
“Tunataka wawekezaji wajue wana wajibu wa kuchangia shughuli za maendeleo kwenye vijiji vinavozunguka maeneo uwekezaji,” alisisitiza.
Makaa ya mawe yamekuwa bidhaa muhimu na adhimu, uwekezaji umeendelea kukua na masoko yameongezeka, wawekezaji waangalie ajira zile zinazosaidia kuendesha miradi yao ili kutoa kipaombele katika maeneo ya vijjiji vilivyozunguka mradi, alisema Waziri Mhagama.
“Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan amefanya kazi nzuri ya kuvutia Wawekezaji Mbalimbali, Wawekezaji wa shamba la Miwa, Wawekezaji wa Makaa ya Mawe, na Wawekezaji wa Umeme wa Maji, naomba kila Muwekezaji aliyeomba ardhi ya uwekezaji atumie kama alivyoomba,”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Mhe. Menas Komba amesema uwekezaji wa Makaa ya Mawe kuna mpango kabambe ambao umelenga kupata asilimia moja ya kila awamu ya mauzo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho akizungumza na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Mhe. Menas Komba (Kulia) wakati wa Mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nakawale.
“Tuendele kushirikiana na wawekezaji wanaokuja kuwekeza ili waendelee kutusaidia na Halmashauri itasimamia kupata haki za wananchi” alisema Mhe. Komba
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Mwalimu Neema Maghembe amesema wawekezaji wote waliowekeza katika Halmashauri ya Songea wamefuata taratibu zote za uwekezaji.
“Tunawawekezaji wa kutosha, wengine wanaendelea na kazi za tafiti mbalimbali na wengine wako katika hatua ya kuanza uchimbaji wa makaa ya mawe”, alisema Mwalimu Maghembe