Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt.
Selemani Jafo ameonesha kuridhishwa na uzingatiaji wa Kanuni na Sheria ya
Mazingira katika Bandari ya Mtwara.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Jafo ya kukagua shughuli za
uhifadhi wa mazingira eneo la utunzaji na usafirishaji wa makaa ya mawe
zinazofanyika katika bandari hiyo.
Ameupongeza uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
mkoani humo kwa kushirikiana na Kampuni ya Ruvuma Coal kwa hatua ya
kulinda mazingira.
Aidha, Waziri Jafo amesema ameridhishwa na namna ambavyo wameweka uzio
kuzunguka eneo yanapohifadhiwa makaa ya mawe ili kudhibiti vumbi lisisambae
na kuathiri wananchi.
“Binafsi nikiwa na dhamana ya kusimamia sekta ya mazingira nimeridhika kwani
mmetekeleza maelekezo yangu niliyoyatoa nilipofanya ziara katika siku
zilizopita,” amesema Dkt. Jafo.
Katika hatua nyingine, Waziri Jafo amewaelekeza wasafirishaji wa makaa ya
mawe kuhakikisha malori yanayosafirisha bidhaa hiyo yanafunikwa kwa turubai ili
kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Akiwa katika eneo la kuhifadhia makaa ya mawe ya Kampuni ya Jitegemee
Holdings, alisema ni lazima malori yote yafunikwe kwa kutofanya hivyo
kunasababisha vumbi katika mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuruhusu biashara.
Pia, amemshukuru kwa kuruhusu Bandari ya Mtwara kutumika kusafirishia
bidhaa ya makaa hayo yam awe akisema kuwa inaliingizia taifa kipato na kukuza
uchumi.
Kuhusu maelekezo yaliyotolewa na Waziri Jafo, Ahmed ameahidi kwa
kushirikiana na wataalamu kutoka ofisi yake kuwasimamia wawekezaji ili kuwa
na biashara isiyo na madhara kwa wananchi.
Nae Meneja Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda
ya Kusini Mhandisi Boniphace Guni ameahidi kusimamia agizo hilo ili liweze
kutekelezeka kwa muda uliopangwa wakati Meneja wa Mgodi wa Makaa ya
Mawe wa Jitegemee Bw. Boscow Mabena ameahidi kuwa watafuata ushauri wa
wataalamu ili kudhibiti uharibifu wa mazingira.
Itakumbukwa Desemba 20, 2021 Waziri Jafo alipofanya ziara bandarini hapo
alitoa muda wa miezi sita kwa uongozi kufanya marekebisho ya dosari za
kimazingira zilizobainika ikiwemo kuandaa eneo maalumu lililokidhi vigezo
litakalotumika kuhifadhi makaa ya mawe yanayosafirishwa.