KITAIFA

TANZANIA, ALGERIA ZASAINI HATI 8 ZA MAKUBALIANO NA MIKATABA YA USHIRIKIANO

TANZANIA, ALGERIA ZASAINI HATI 8 ZA MAKUBALIANO NA MIKATABA YA USHIRIKIANO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika mafunzo ya diplomasia kati ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania (CFR) na Chuo cha Diplomasia cha Algeria wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesaini Hati 8 za
Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta za umeme, gesi,
biashara, viwanda na kilimo, utamaduni na sanaa,
kumbukumbu na nyaraka, mafunzo katika vyuo vya
diplomasia na ushirikiano katika taaluma na teknolojia.
Utiaji saini wa makubaliano hayo umeshuhudia na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya
Nje na Diaspora wa Algeria wakati wa Mkutano wa Tano
wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya
Tanzania na Algeria.
Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano Ngazi ya
Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 30 hadi 31 Julai
2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria. Pembeni yake ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo.


Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huu umeongozwa
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax. Viongozi wengine
waliohudhuria ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Dkt. Seif Shekalaghe na Naibu Makatibu Wakuu kutoka
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mambo ya Ndani
ya Nchi, na Nishati.
Madhumuni ya mkutano huo ni kutathmini hatua iliyofikiwa
katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya ushirikiano
yaliyokubaliwa kwenye Mkutano wa Nne uliofanyika
mwaka 2010 jijini Dar es Salaam.

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri
Tax ameleza kuwa mkutano huu ni kielezo cha dhamira ya
dhati kati ya Tanzania na Algeria kuendelea kuimarisha
ushirikiano uliopo na kuweka mfumo rasmi wa kujitathimini
katika masuala mbalimbali yaliyokubalika.
‘’ Ni imani yangu kuwa wataalam wetu wamefanya kazi
kubwa katika majadiliano kwa kuangalia maeneo muhimu
na ya kipaumbele ili kuendelea kukuza ushirikiano kwa
maslahi ya nchi zote mbili” alisema Dkt. Tax.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria,
Mhe. Ahmed Attaf katika hotuba yake ameeleza kuwa 
mkutano huo umetoa fursa ya kujadili na kukubaliana
maeneo ya kipaumbele kwa maslahi ya pande mbili. 
Pia ameeleza kuwa kusainiwa kwa makubaliano ni ishara
ya wazi kuwa nchi hizi zitaendelea kudumisha uhusiano
mzuri uliopo sanjari na kukuza ushirikiano kwenye
maeneo mapya yenye tija. 
‘’Serikali ya Algeria itaendelea kushirikiana kwa karibu na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kufanya kazi pamoja ili kufikia malengo tuliyojiwekea
katika sekta mahsusi za ushirikiano,’’ alisema Mhe. Attaf.

Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Attaf wamewashukuru Wakuu wa
Nchi wa pande zote mbili kwa utayari na jitihada zao
wanazozifanya katika kuhakikisha ushirikiano uliopo
unaimarishwa zaidi kwa maslahi mapana ya nchi mbili.

Mkutano huo umejadili na kutathimini utekelezaji wa
maeneo ya ushirikiano katika Siasa na Diplomasia, Ulinzi
na Usalama, Fedha na Uchumi, Nishati, Habari na
Mawasiliano, Kilimo, Elimu na Mafunzo, Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi na Afya, na
Sanaa na Utamaduni.
Katika kuendelea kuhakikisha kwamba Tanzania na
Algeria zinatekeleza maazimio ya mkutano husika, nchi
hizi mbili zimekubaliana kuitisha mkutano wa sita
utakaofanyika nchini Tanzania mwaka 2025.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *