Wananchi wa Newala wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipopewa fursa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuzungumza nao walipokusanyika eneo la Stendi ya Mabasi ya Newala.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi
amesema Serikali ya Awamu ya Sita itajenga wodi ya mama na mtoto ya
kisasa katika Hospitali ya Wilaya ya Newala ili kuboresha utoaji wa huduma
ya afya ya uzazi.
Mhe. Ndejembi amesema hayo akiwa katika Wilaya ya Newala, mara
baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Kassim Majaliwa kumpatia fursa ya kuzungumza na wananchi wa eneo
hilo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nambunga alipopewa fursa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuzungumza na wananchi hao.
Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, wodi hiyo ikikamilika itawawezesha
wananchi kupata huduma za kisasa badala ya kusafiri umbali mrefu
kufuata huduma katika hospitali ya rufaa ya mkoa.
Sanjari na hilo, Mhe. Ndejembi amesema Serikali imetoa shilingi milioni
600 katika jimbo la Newala Mjini kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya viwili
kwa gharama ya milioni 250 kwa kila kituo, ikiwa ni pamoja na zahanati
moja itakayogharimu shilingi milioni 100.
Ameongeza kuwa, Serikali imetoa gari mbili za wagonjwa (Ambulance)
pamoja na gari lingine atakalokuwa akilitumia Mganga Mkuu wa Wilaya
kutembelea zahanati na vituo vya afya ili kuhimiza utoaji wa huduma bora
kwa wananchi.
Aidha, Mhe. Ndejembi ameanisha kuwa Halmashauri hiyo ilikuwa
ikikabiliwa na changamoto ya baadhi ya kata kukosa shule ya Sekondari
lakini kiasi zaidi ya bilioni 209 kilichotolewa na Rais Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa ajili ya kujenga shule za sekondari nchini
kimeiwezesha Halmashauri hiyo kupata shule katika kata zake.
“Hapa Newala mmepata milioni 560 ya kujenga shule mpya ya sekondari
ambayo ujenzi wake unaendelea na katika mwaka wa fedha uliopita
mlipata shilingi milioni 470 za ujenzi wa shule na kwasasa imebaki kata
moja tu kupata shule lakini Serikali inatafuta fedha ili kujenga shule katika
kata hiyo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
amehitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili katika Wilaya za Tandahimba na
Newala iliyolenga kukagua ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu
ambayo inajengwa ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.