Jeshi la Polisi kupitia chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) kimeandaa mashindano ya Polisi Jamii yatakayo shirikisha wananchi pamoja na askari wa Jeshi hilo lengo likiwa ni kuwaleta karibu wananchi na Jeshi la Polisi katika kutokomeza uhalifu na kuchangia damu katika benki ya damu salamu.
Akizungumza na vyombo vya habari chuoni hapo leo Agosti 15, 2023, Mkuu wa Chuo hicho,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Dkt. Lazaro Mambosasa, amesema lengo la mashindano hayo ni kuwashirikisha wananchi katika michezo ambayo itawakutanisha na askari wa Jeshi la Polisi ambapo watabadilishana taarifa mbalimbali zikiwemo za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao.
Mbali na burudani itakayotolewa na michezo hiyo, pia Jeshi hilo kupitia wakufunzi na wanafunzi wa chuo hicho pamoja na washiriki wengine kutoka nje ya chuo hicho wanakusudia kuchangia damu katika benki ya damu salama, zoezi ambalo linatarajiwa kusimamiwa na hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Temeke.
Kwa upande wake Afisa Michezo wa chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Salum Madongo amesema katika mashindano hayo wanatarajia kuhusisha michezo Kumi na Sita ikiwemo mpira wa miguu kwa wanaume na wanawake, mpira wa Wavu, Masumbwi, Taekwondo, Judo, riadha na kadhalika.
Naye Kocha wa mpira wa kikapu Lincon Kagame, amesema wamefarijika kualikwa na kushiriki michezo ya Polisi Jamii ambapo amebainisha kuwa michezo hiyo itawaleta karibu na kuwaunganisha na jeshi la Polisi katika kupambana na uhalifu.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuzinduliwa tarehe 25 Agosti 2023 ambapo itakuwa siku ya ugawaji wa vifaa mbalimbali kwa timu zote shiriki Pamoja na zoezi la uchangiaji wa damu na Septemba 04 yataanza rasmi na kumalizika Septemba 23.