Na Mwandishi Wetu
DODOMA. Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu itaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli unaimarishwa kwa kutenga fedha kila mwaka ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo ya ndani na nje ya Tanzania inayosafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza katika Kikao cha Utatu kilichojumuisha Balozi wa China, Waziri wa Uchukuzi wa Serikali ya Tanzania na Waziri wa Uchukuzi na Lojistiki wa Serikali ya Zambia kilichofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma, Waziri Mbarawa amesema kuimarisha kwa usafiri wa reli wa nchini hususani Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kutapunguza changamoto za usafirishaji wa mizigo hususani kwa mizigo inayokwenda Zambia na Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
“Kufanyika kwa kikao ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Rais Wa Tanzania na Zambia katika kuhakikisha TAZARA inafufuliwa upya na hapa tumejadiliana njia bora zaidi za kulifufua upya ambapo tayari kamati zilizoundwa zinaendelea na kazi na zitawasilisha ripoti kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi’ amesema Waziri Mbarawa.
Waziri Mbarawa ameongeza kuwa kwa sasa tayari kamati tatu zimeshaundwa ili kujadili namna bora ya kuimarisha Shirika la Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuhakikisha shirika hilo linasafirisha mzigo mwingi zaidi.
Kwa upande wake Balozi wa China chini, Chen Mingjian amesema Serikali ya china kama sehemu ya mdau mkubwa wa reli hiyo iko tayari kuhakikisha shirika hilo linaboreshwa ili kutoa mchango kwa nchi na kurahisisha usafirishaji wa mizigo.
Naye Waziri wa Uchukuzi na Lojistiki wa Zambia Frank Tayali amemuhakikishia Waziri Mbarawa na Balozi Chen kuwa Zambia imejipanga na tayari kama sehemu ya mbia wa Shirika hilo inaendelea kutekeleza makubaliano mbalimbali yaliyoingiwa baina ya Tanzania na Zambia lengo likiwa kulifufua upya shirika hilo.
1 Comment
Hello. remarkable job. I did not imagine this. This is a remarkable story. Thanks!