KITAIFA BIASHARA

MWANGA MPYA: TARURA YAPELEKA ZAIDI YA SH50BILIONI MRADI WA BARABARA MKOANI IRINGA

MWANGA MPYA: TARURA YAPELEKA ZAIDI YA SH50BILIONI MRADI WA BARABARA MKOANI IRINGA

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji wa Barabara za Vijijini kwa Ushirikishaji na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi “Roads to Inclusion and Social Economic Opportunities (RISE)” katika mkoa wa Iringa lengo likiwa ni kujenga barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Kilomita 33 ili wananchi waweze kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi pamoja na kusafirisha mazao kwenda sokoni.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor H. Seff wakati wa ziara ya Kamati ya Ufundi ya mradi wa RISE ilipofanya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Wenda–Mgama yenye urefu wa Km 19 iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na ujenzi wa barabara ya Mtili–Ifwagi yenye urefu wa Km 14 iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ambapo zote zinajengwa kwa kiwango cha lami na tayari wakandarasi wote wamefika eneo la kazi ( Site) ambapo hatua za awali za utekelezaji ‘’mobilization ‘’ zimeanza.

‘’Leo nimefanya ukaguzi wa mradi wa RISE nikiwa nimeambatana na Kamati ya Ufundi ya mradi na lengo kuu hasa ni kuhakikisha mpango uliowekwa kati ya TARURA na Makandarasi wanaotekeleza mradi huo wanatekeleza kama ilivyopangwa na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati kulingana na mkataba na kama kuna changamoto yoyote ifahamike na kutatuliwa kwa wakati ili miradi yote ikamilike mapema na kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa’’, alisema Mhandisi Seff.

Aidha, Mhandisi Seff amemuagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Iringa kuhakikisha anasimamia kwa karibu mikataba ya mradi huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mahitaji yote na maandalizi yanakamilika kwa wakati ili mradi huo ukamilike kwa muda na uweze kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Pia, Mhandisi Seff amewasisitiza wananchi wanufaika wa mradi huo kujitokeza kuunda vikundi kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara kwani watakuwa wanalipwa ili kujiongezea kipato na amewataka wahudhurie mafunzo yatakayokuwa yanatolewa chini ya mradi ili waendelee kulinda barabara ziweze kuwasaidia katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inatekeleza mradi wa RISE unaolenga uboreshaji wa barabara za vijijini kwa ushirikishaji na ufunguaji wa fursa za kijamii na kiuchumi kwa wananchi “Roads to Inclusion and Social Economic Opportunities (RISE)” katika mikoa minne ambayo ni Mkoa wa Iringa, Geita, Tanga na Lindi.

About Author

Bongo News

29 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *