Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewataka wavuvi kuchangamkia fursa iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ya ugawaji wa boti na vizimba ili waweze kufanya shughuli zao kisasa na kuboresha maisha yao.
Waziri Ulega ametoa rai hiyo alipofanya ziara katika Soko la Samaki la Kimataifa la Kilumba mkoani Mwanza, alipowatembelea wavuvi hao kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.
Amesema fursa hiyo ya vifaa vya kisasa aliyoitoa Rais Samia wakiitumia vizuri na wakafanya uvuvi na ufugaji wa kisasa wa samaki aina ya Sato itasaidia Ziwa Victoria kupumua na samaki aina ya Sangara na Dagaa kuongezeka na kuinua uchumi wao.
“Tutumie fursa hiyo vizuri, tuzalishe vya kutosha ili Rais aone umuhimu wa kutuongezea vyombo vingine vya kisasa kwa sababu yeye anachokifanya ni kutuwekea mazingira mazuri ili tuendelee kunufaika na shughuli zetu”. Amesema Waziri Ulega