Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Novemba 19, 2023 amepokea msaada wa vifaa tiba vya thamani ya Milioni 137 kutoka katika Familia ya GSM vifaa tiba ambavyo vimeelekezwa katika Taasisi ya ocean road Jijini Dar es Salaam.
Siku ya leo imekuwa muhimu na maalum kwa familia ya mmiliki wa GSM Bwana Gharib Mohamed ndio siku aliyo zaliwa ambapo ameitumia siku hiyo kama Kumbukizi ya kuzaliwa kwake kutoa msaada wa vifaa tiba katika Taasisi ya ocean road
Akipokea msaada huo RC Chalamila amesema kwa hatua aliyofikia Bwana Gharib Mohamed anachohitaji sasa ni Mungu na Afya njema, “mwezetu GSM ameona ni busara wakati wa Kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa afanye jambo jema kwa wenye uhitaji hususani wagonjwa wa cancer katika Taasisi ya ocean road, cha kujiuliza Je? wewe unapofanya Kumbukizi ya kuzaliwa unafanya nini kwa wenye uhitaji” Alisema Chalamila
Aidha RC Chalamila ametoa rai kwa matajiri wote katika Mkoa wa Dar es Salaam kumheshimisha Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za kuleta maendeleo Katika Jamii. ” Dkt samia Suluhu Hassan amekuwa akiwekeza sana katika sekta ya Afya kwa kutambua umuhimu wake hata hivyo tayari ameshaidhinisha ununuzi wa mashine ya kisasa katika Taasisi ya ocean road ambayo muda si mrefu itaanza kutoa huduma” alisisitiza Mhe Chalamila
Kwa upande wa Dkt Julius Mwaisilage wa Ocean road amesema msaada wa vifaa tiba hivyo umekuja muda muafaka kutokana na uhitaji mkubwa wa vifaa hivyo katika Taasisi ya Ocean road hivyo amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuvisimamia vizuri vifaa hivyo ili viweze kutoa huduma katika hali ya ubora kwa Kipindi kirefu
RC Chalamila amesema Fedha hupotea lakini matendo hudumu alichokifanya Bwana Gharib Mohamed na familia yake kitaendelea kudumu aidha ifahamike kuwa GSM ndiye mdhamini mkubwa wa timu ya mpira Young African lakini hajaishia kwenye michezo tu ameendelea kuunga mkono katika sekta ya Afya hapa nchini.