*Akerwa na viongozi Mwanza kutofanyia kazi agizo la Makamu wa Rais*
*Amwagiza Waziri wa Ardhi kwenda jijini Mwanza kutatua kero ya muda mrefu*
*Aweka jiwe la Msingi ujenzi wa Makao Makuu AICT*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka viongozi wa Serikali katika maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha wanatatua kero za wananchi kwa wakati badala ya kuzichukua bila ya kuzifanyia kazi.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Hafla ya kuweka jiwe la msingi jengo la Ofisi za Makao Makuu ya Africa Inland Church Tanzania ( AICT) Jijini Mwanza.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo kufuatia risala ya Askofu Mkuu AICT, Mussa Magwesela liyoweka wazi kasi nsogo ya utatuzi wa changamoto zinazolitatiza Kanisa hilo kwa muda mrefu bila kupatiwa majibu wala utatuzi.
Dkt. Biteko amesema mbali na agizo la Makamu wa Rais, Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango la kushughulikia hoja ya AICT kuhusu umiliki wa Shule za Sekondari za Bulima na Kahunda pamoja kiwanja kilichopo jijini Mwanza katika eneo la Makongoro lakini agizo hilo bado halijashughulikiwa.
” Hili suala la Kahunda na Bulima nataka niwahakikishie kwamba tunalitambua na tunalifanyia kazi, lakini hili la umiliki wa kiwanja sifurahishwi na kasi ya ndogo ya ushughulikiaji, haiwezekani jambo hili
kutoka Makamu wa Rais alitolee maelekezo mwezi Januari mwaka 2023 hakuna majibu hadi leo, kama ombi la Kanisa haliwezekani au linawezekana wapeni majibu wahusika.” Amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko amemwagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kukutana chini usimamizi wa Mkuu wa Mkoa siku ya Ijumaa (tarehe 22 Machi 2024) washughulikie suala hilo na wahusika wapewe majibu ya changamoto husika.
Kuhusu ombi la AICT la kulipwa fedha wanazodai Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) takribani shilingi milioni 181, Dkt. Biteko amesema kuwa kabla ya mwisho wa mwezi huu fedha zote zitakuwa zimelipwa na hii ni baada ya kufanya mazungumzo na Wizara ya Afya.
Aidha kuhusu ombi la kanisa hilo la kuwekewa mfumo wa majitaka amesema kuwa, litafanyiwa kazi kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza ( MWAUWASA).
Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua kuwa Serikali peke yake haiwezi kupeleka maendeleo kwa wananchi wote kwa wakati hivyo madhehebu ya dini yana mchango wake katika maendeleo.
Amesema Rais anatambua kuwa ili kuwa na jamii ya watu waliostaarabika na kuheshimika elimu ni jambo la msingi lakini pia nyumba za ibada zina umuhimu mkubwa katika kukuza watu kimaadili.
Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia yupo tayari muda wowote kuwasilikiza viongozi wa dini na kuchukua ushauri wao na kwamba anaamini katika maridhiano na kujenga Taifa lenye umoja.
Awali, Baba Askofu Mkuu wa AICT, Mussa Magwesela alisema kuwa, Kanisa linatambua juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi pamoja na ustawi wa kijamii na hivyo AICT itaendelea kuunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ikiwemo kwenye Elimu na Afya pamoja na kuendelea kuhubiri amani, mshikamano na umoja.
Amesema kuwa, Kanisa hilo pia linaendelea kutoa elimu ya ujasiriamali katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwakwamua wananchi kiuchumi, kwani AICT inatambua kuwa mwanadamu si roho pekeyake bali ana mwili wenye mahitaji mbalimbali.
Ameongeza kuwa, AICT pia itaendelea kushikamana na Serikali katika kupinga vitendo vyote ambavyo ni kinyume na maadili ya kitanzania.
Vilevile Askofu Magwesela amesisitiza kuhusu umoja, uwazi, uwajibikaji, uadilifu na uaminifu katika utendaji kazi wa kila siku ili kutekeleza kwa ufanisi mipango inayowekwa ndani na nje ya Serikali.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangira, Maaskofu wa AICT kutoka Dayosisi zote 7 nchini na Baraza la Utendaji la Kanisa AICT.
Kanisa la AICT lilianzishwa miaka 115 iliypita na Makao yake Makuu yakiwa ni Mkoani Mwanza.