Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi hilo kutekeleza majukumu yake.
Meja Jenerali Mabele ameyasema hayo wakati akihitimisha zoezi la ufungaji wa mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT katika Kikosi cha Rwamkoma JKT kilichopo Wilaya ya Butiama mkoani Mara.
“Serikali imekuwa ikiboresha miundo mbinu ya Makambi na Vikosi vya JKT ili kuliwezesha Jeshi hili kuchukua vijana wengi zaidi kwa ajili ya kupatiwa mafunzo”. Aliongeza Meja Jenerali Mabele.
Kando na hilo, Meja Jenerali Mabele amepata wasaa wa kuzindua rasmi mitandao ya kijamii ya JKT ambayo ni Twitter, Instagram na Facebook ili kuupa wigo Umma wa watanzania kupata habari mbalimbali zinazohusu JKT.
“Kwakuwa dunia kwa Sasa ipo kiganjani hivyo nasi JKT tunalitambulisha jukwaa la mitandao yetu ya kijamii kuwa moja ya eneo ambalo jamii itaweza kupata habari zetu kwa uhakika, mbali na ile njia ya Tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz inayoendelea kutumika.”
Amefafanua kuwa mitandao hiyo ya kijamii itasaidia upatikanaji wa taarifa na maelekezo mbalimbali yanayohusu matangazo ya Vijana wa Kujitolea na yale ya Mujibu wa Sheria.
Akitoa salamu za Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda, Mkurugenzi wa Utumishi kutoka Tawi la Utumishi Jeshini Brigedia Jenerali Simon Pigapiga amewataka wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri na kujiepusha na vitendo viovu.
“Niwasihi mkawe vijana bora wakati wote kwa kujiepusha na vitendo viovu vitakavyowasababishia matatizo ya afya ya mwili na akili”. Alisema Brigedia Jenersli Pigapiga.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar, Kanali Makame Daima amesema kuwa JKU inaendelea kujifunza kutoka kwa JKT kutokana na ushirirkiano uliopo baina ya vyombo hivyo viwili.
“Nimekuwa nikipokea maelekezo toka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuitaka JKU kuwa kama JKT, nami natekeleza agizo hilo kwa vitendo”. Aliongeza Kanali Daima.
Akitoa taarifa ya mafunzo ya Kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT, Mkuu wa Tawi la Mafunzo na Operesheni JKT Kanali Aisha Matanza amesema mafunzo hayo yamechukua jumla ya majuma 16 mfululizo.
“Vijana hawa wanawawakilisha vijana wenzao ambao wamefanya mafunzo kama haya katika vikosi vingine vya JKT”. Aliongeza Kanali Matanza.
Kwa upande wake Kamanda Kikosi Luteni Kanali Gaudencia Mapunda amesema mafunzo waliyoyapata vijana hao yamewajengea Uzalendo, Uadilifu na uwajibikaji kwa Taifa lao.
” Hadi kufikia hii leo wahitimu hawa wamefikia malengo yao ya mafunzo haya kwa kiwango cha juu”. Aliongeza Kanali Mapunda.
Akisoma risala mbele ya mbele ya mgeni rasmi kwa niaba ya wahitimu wenzake, Service Girl Irimina Adolph amesema mafunzo ya JKT waliyoyapata wamefaikiwa kujengewa uzalendo, Nidhamu, Ukakamavu na Umoja wa Kitaifa, Vilevile yamewajenga katika nyanja mbalimbali kama vile kilimo cha mazao mbalimbali pamoja na shughuli za ufugaji na uvuvi kwa kutumia zana za kisasa.
Mafunzo ya Vijana wa JKT kwa Kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT yalifunguliwa katika Makambi yote ya Mafunzo Desemba 27, 2023 na yamehitimishwa rasmi leo na Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele.
Baada ya Mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa Kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT kuhitimishwa katika makambi 19 vijana hao wanatawanywa na kwenda kuanza hatua nyingine ya mafunzo ya stadi za kazi na stadi za maisha katika vikosi mbalimbali kwa muda wa miezi 20 ili kukamilisha miaka miwili ya mkataba wao na JKT.