Dar es Salaam: Mahakama ya Rufani imeamuru kesi ya mgogoro wa malipo ya mkopo wa Dola za Marekani 18.64 milioni (zidia ya Sh47 bilioni) baina ya kampuni ya State Oil Tanzania dhidi ya Equity Bank Tanzania Limited (EBT) na Equity Bank Kenya Limited (EBK) ianze upya kusikilizwa.
Mahakama hiyo imeamuru kesi hiyo ianze upya baada ya kubatilisha hukumu iliyopita ushindi kampuni ya State Oil, iliyotolewa na Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara katika kesi ya kibiashara namba 105 ya mwaka 2020.
Imebatilisha hukumu hiyo baada ya kubaini kasoro katika mwenendo wa kesi hiyo, kuwa mahakama hiyo Iliendelea kusikiliza na kuamua kesi hiyo bila hati ya madai kufanyiwa marekebisho baada ya wadaiwa kuongezeka kutoka mmoja na kuwa wawili.
Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye (Kiongozi wa jopo), Abraham Mwampashi na Zainabu Muruke, Alhamisi, Mei 16, 2024, kutokana na rufaa iliyokatwa na benki hizo, za EBT na EBK.
Kutokana na kasoro hiyo ya kutokutolewa amri ya kurekebisho ya hati ya madai, Mahakama hiyo imesema ku kuwa katika mazingira ya kesi hiyo kutokutolewa amri ya marekebisho ya hati ya madai baada ya EBK kuongezwa katika kesi kama mdaiwa wa pili, ilikuwa ni kasoro kubwa isiyorekebishika.
Mahakama hiyo imesema kuwa kasoro hiyo inavunja masharti ya lazima ya Amri ya 1 Kanuni ya 10 (4) ya Sheria ya Kanuni za Madai (CPC) na kwamba pia kumeathiri mwenendo na vilevile hukumu iliyotokana na Mwenendo huo.
“Tunabatilisha mwenendo wote uliotokana na amri hiyo”, imesema Mahakama ya Rufani, katika uamuzi wake ulioandikwa na Jaji Mwampashi kwa niaba ya jopo la majaji hao na kuhitimisha:
“Pia tunatengua hukumu na kurejesha kumbukumbu (jalada) za kesi ya kibiashara namba 105 ya mwaka 2020, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwa ajili ya kesi kusikilizwa upya baada ya kukidhi matakwa ya Amri ya 1 Kanuni ya 10 (4) ya CPC”.
Awali State Oil ilifungua kesi hiyo dhidi ya EBT, kama wakala wa EBK, kufuatia mgogoro wa malipo ya mkopo wa Dola za Marekani 18,640,000 ambazo EBK inaidai State Oil.
Kabla kesi hiyo kuanza kusikilizwa, mawakili wa EBT waliziomba mahakama iamuru EBK nayo iunganishwe katika kesi hiyo kama mdaiwa wa pili kwa kuwa nayo Ina maslahi katia kesi hiyo na Mahakama ikakubaliana na ombi hilo na ikaamuru EBK iwasilishe maelezo yake ya utetezi wa maandishi.
Hata hivyo licha ya wadaawa kuongezeka yaani EBK na hivyo wadaiwa kuwa wawili badala ya mmoja, Mahakama Kuu haikuamuru hati ya madai ifanyiwe marekebisho ili kuakisi mabadiliko hayo ya wadaawa yaani kuitaja EBK katika hati ya madai kama mdaiwa wa pili.
Badala yake iliendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo kwa kutumia hati ya madai ya awali ya wadaawa wawili na ikaipa ushindi State Oil, ndipo benki hizo zote mbili EBT na EBK zikakata rufaa Mahakama ya Rufani kuupinga hukumu hiyo.
Siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo Aprili 13, 2024, kabla ya kuanza usikilizwaji Mahakama iliibua kasoro hiyo, ikahoji iwapo ilikuwa sawa Mahakama Kuu kusikiliza na kuamua kesi hiyo bila kwanza kuamuru kufanyika kwa marekebisho ya hati ya madai baada ya mabadiliko ya wadaawa.
Mawakili wa pande zote mbili, Mpaya Kamara na Timon Vitalis wanaowawakilisha warufani (benki hizo) na Frank Mwalongo anayeiwakilisha State Oil, pamoja na mambo mengine waliieleza mahakama kuwa, haikuwa muhimu kufanya marekebisho hayo kwa kuwa hayakuuathiri upande wowote.
Hata hivyo Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake imesema kuwa kwa kuzingatia asili ya mgogoro baina ya wadaawa na kiasi cha pesa kinachohusika kuwa kikubwa, hitaji la usikilizwaji sawa ambalo ni kwa mujibu wa matakwa ya lazima ya taratibu za kisheria, hati ya madai ilipaswa kurekebishwa kukidhi matakwa ya lazima ya Amri ya 1 Kanuni 10 (4) ya CPC.
Imesema kwamba kutofanya marekebisho hayo State Oil haikuwa na kesi au madai dhidi ya EBK na kwamba mbali na madai kinzani iliyoyatoa katika maelezo yake ya utetezi wa maandishi, EBK iliishia kutetea kesi iliyooelekezwa kwa EBT tu.
Kwa mujibu wa kumbukumhu za kesi hiyo mwaka 2018 Benki ya Equity Kenya ilizidhamini State Oil kupata mkopo wa Dola za Marekani 18.64 milioni kutoka kampuni ya Lamar Commodity Trading DMMC ya Dubai, huku State Oil yenyewe Ikiweka dhamana zake kwa EBK, chini ya usimamizi wa EBT.
Hata hivyo State Oill ilipuuza kulipa mkopo huo hivyo mdhamini wake EBK ikalazimika kuulipa, na EBT ikaidai State Oil deni hilo kwa niaba ya EBK, ndipo State Oil ilipokimbilia mahakamani.
Katika kesi hiyo kampuni hiyo iliiomba mahakama iiamuru EBT iirejeshee hati za mali ilizokuwa imeziweka dhamana, kwa ajili ya kupata udhamini kutoka kwa EBK, huku ikidai kuwa haidaiwi na benki hizo, kwa madai kuwa EBK haikuidhamini kupata mkopo huo.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo mwakilishi wa kampuni ya Lamar iliyotoa mkopo huo alieleza kuwa iliipa State Oil mkopo huo baada ya kudhaminiwa na EBK na kwamba ukishindwa kuurejesha, hivyo mdhamini wake, EBK ndo akaulipa.
Hata hivyo mahakama hiyo katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Stephen Magoiga Oktoba Mosi, 2021, alikubaliana na madai ya State Oil, kuwa ilikuwa imeshalipa deni lake lote na hivyo benki hizo hazikuwa na madai dhidi yake.
Hivyo jaji Magoiga aliamuru hati za mali zote zilizokuwa zimewekwa dhamana na State Oil, zinashikiliwa zirejeshwe kwa kampuni hiyo.
Mwisho