Dar es Salaam: Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imeshindwa kuendelea na usikilizaji wa kesi ya mgogoro wa malipo ya mkopo dhidi ya Benki za Equity Bank Tanzania na Equity Bank Kenya, badala yake sasa imepangwa kuunguruma kwa siku nne mfululizo, kuanzia Septemba 2 mpaka 5, 2024.
Kwa siku hizo zote shahidi wa pili wa upande wa madai atakuwa katika kikaango cha maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa utetezi katika kesi hiyo.
Kesi hiyo imefunguliwa na kampuni ya Continental Reliable and Clearing (CRC) dhidi ya benki hizo, ambapo kampuni hiyo ikipinga kudaiwa kurejesha mkopo huo.
Kampuni hiyo inadaiwa na benki hizo marejesho ya mkopo wa zaidi ya Dola za Marekani 10.13 milioni ilizokopeshwa na benki hizo.
CRC ilifungua kesi hiyo baada ya benki ya EBK kupitia wakala wake, EBT kuiandikia barua ikiipa siku 21 kurejesha mkopo wake uliotolewa kwake kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2013, Dola za Marekani 10,139,664.95 (yaani Dola 10.13 milioni, sawa na zaidi ya Sh26 bilioni).
Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 16 ya mwaka 2023 inayosikiliizwa na Jaji Profesa Agatho Ubena, CRC inadai kuwa ilisharejesha mkopo wote na hivyo haina deni kwa benki hizo.
Kesi hiyo iko kwenye hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa madai na sasa ikiwa inaendelea kupokea ushahidi wa shahidi wa pili wa madaii
Kesi ilipangwa kuendelea kusikilizwa mahakamani hapo kwa siku mbili mfululizo yaani jana na leo.
Hata hivyo jana ilikwama kwa kuwa Jaji Profesa U ena anayesikiliza hakuwepo , na hivyo iliahirishwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo Joyce Minde, hadi tarehe hizo.
Kesi hiyo ilipoitwa kwa Msajili kwa ajili ya ahirisho hilo, wakili wa mdai, Frank Mwalongo ameomba wapangiwe kuendelea siku ya kesho lakini Naibu Msajili Minde amesema kuwa hata kesho Jaji Ubena hatakuwepo, ndipo Wakili Mwalongo akaiomba hizo tarehe za Septemba.
Kesi hii ni miongoni mwa kesi kadhaa zilizofunguliwa na kampuni mbalimbali zikipinga kudaiwa na benki hizo na zile zilizofunguliwa na benki hizo dhidi ya kampuni kadhaa zikizidai kampuni mbambali pesa ambazo znadai zilizikopesha mabilioni ya fedha, lakini zimeshindwa au zimepuuza kurejesha mikopo hiyo.
Mara ya mwisho Mahakama hiyo iliikatalia kampuni hiyo kupokea nyaraka muhimu katika.utetezi wake kutoka na kutokutomiza matakwa ya kisheria.
Kampuni hiyo kupitia shahidi wake wa pili, Alexander Gombanila akiongozwa na Wakili wa kampuni hiyo, Mwalongo, iliiomba mahakama hiyo ipokee nyaraka hiyo iliyodaiwa kuwa ni jedwali la malipo ya mkopo wote ambao kampuni hiyo ilipewa na benki hizo.
Hata hivyo mawakili wa benki hizo, Emmanuel Saghan anayeiwakilisha EBT ( mdaiwa wa kwanza) na Mpaya Kamala, anayeiwakilisha EBK (mdaiwa wa pili) walipinga nyaraka hiyo kupokewa wakidai kuwa haijakidhi matakwa ya kisheria.
Mahakama katika uamuzi wake ilikubaliana na hoja za pingamizi la mawakili wa utetezi ikaitupilia mbali nyaraka hiyo.
Baada ya hatua hiyo mawakili hao wa utetezi walianza kumhoji shahidi hugo maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake aliokwishauwasiliaha mahakamani hapo kwa njia ya maandishi pamoja na nyaraka mbalimbali wanazokusudia kutumika kama vielelezo vya ushahidi.
Aliyeanza kumhoji shahidi huyo ni Wakili Saghan ambapo pamoja na mambo mengine shahidi huyo alieleza kuwa yeye hakuwepo wakati mkopo huo inatolewa kwani alikuwa bado hajaajiriwa katika kampuni hiyo.
Badala yake alidai kwamba taarifa alizozitoa kuhusiana na mkopo huo ni zile alizozisikia kwa wafanyakazi wenzake na alizozikuta ofisini. Hata hivyo hakumaliza maswali yake ndipo kesi hiyo ikaahirishwa mpaka jana na leo.
Kwa hiyo itakakapoendelea mawakili hao wa utetezi wataendelea kumhoji shahidi huyo maswali mbalimbali.