WATU Sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Tanga wakituhumiwa mauaji ya Watu watatu akiwemo aliyekuwa mkaguzi wa ndani ‘Internal Audit’ wa Halmashauri ya (W) Korogwe Jonaisa E – Shayo.
Katika tukio hilo la mauaji la tarehe 23/09/2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga ACP Almachius Mchunguzi amethibitisha na kuwataja waliouawa kuwa ni Jonaisa Edward Shayo aliyekuwa mkaguzi wa ndani Halmashauri ya wilaya Korogwe, Bedan Lameck Shayo na Sara Bakari Hassan aliyekuwa dada wa kazi.
Watuhumiwa wa mauaji hayo wanaoshikiliwa na Polisi ni Bernard Adam Kizuguto (31), Mkulima na mkazi wa Msambiazi Korogwe, Marko John Jambia (28) Mkulima na mkazi wa wilaya ya Lushoto.
Wengine ni Peter John Jambia ‘Johnson’ (31) Mkulima wa Msambiazi Korogwe, Hassan Ramadhan Bakari (53) Mkulima na mkazi wa Kwamaraha Handeni na James Mkama ‘Ticha’ (42) ambaye ni mkazi wa Mtonga Korogwe.
Mwingine ni Omari Salehe ‘Mwiba’ (29) Mkulima na mkazi wa Kwamaraha wilayani Handeni na Kamanda ACP Mchunguzi amesema upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili hatua stahiki za kisheria kuweza kuchukuliwa.
Kamanda huyo wa Polisi Mkoa wa Tanga ACP Almachius Mchunguzi ameeleza kuwa Marehemu wote watatu walikuwa wakazi wa Bagamoyo wilayani Korogwe na mauaji yao yalitokea tarehe 23/09/2024 katika eneo la ndani ya msitu wa hifadhi ya Korogwe Kata na tarafa ya Sindeni wilayani Handeni.
Aidha Kamanda huyo wa Polisi (ACP Almachius Mchunguzi) alibainisha kwamba tarehe 23/09/2024 kulitokea tukio la kuchomwa moto kwa gari aina ya Toyota IST lenye nambari T 305 EAL ambapo ndani na nje ya gari hilo iligundulika miili ya watu watatu.
“Miili hiyo ilibainika kuwa ni ya watu hao baada ya kufanyika utambuzi na uchunguzi wa kitaalam, kufuatia tukio hilo Jeshi la polisi limefanya uchunguzi na msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watu Sita”alisema ACP Mchunguzi.
Kwa mujibu wa ACP Mchunguzi, Jeshi la Polisi linalaani vikali vitendo hivyo vya kihalifu na halitamuonea huruma au kusita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu yeyote au kikundi cha watu kinachojihusisha na vitendo vya uhalifu.
Ameendelea kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuweza kubaini na kuzuia uhalifu na kuendelea kuuweka Mkoa wa Tanga katika hali ya Usalama.