Mwalimu Peter Pantaleo, msemaji wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania (TAPSHA) na Jumuiya ya Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), ametoa shukrani za dhati kwa Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, kwa msaada wa majiko 800 ya gesi kwa walimu wa jiji la Arusha

Hafla ya makabidhiano hayo amefanyika Jumatatu, Oktoba 7, 2024, katika Hoteli ya Gran Melia mkoani Arusha. Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwalimu Pantaleo amemshukuru Balozi Chen kwa kuunga mkono ahadi ya Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo, ya kukabidhi majiko 5,000 kwa walimu kama sehemu ya Kampeni ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Majiko utakayotupa leo yatatusaidia sisi walimu wa jiji la Arusha kuunga mkono kampeni iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia ya matumizi ya nishati safi. Mheshimiwa Mbunge anaamini sisi walimu wote tukitumia majiko ya gesi, kampeni hii ya matumizi ya nishati safi itaifikia jamii kubwa kwa urahisi zaidi,” amesema Pantaleo.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania, kupitia Rais Samia, inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa kuleta miradi ya ujenzi wa madarasa, maabara, hosteli, ofisi za walimu, na nyumba za walimu, ambayo imekuwa motisha kwa walimu. Pantaleo pia amesifu ongezeko la mishahara kwa walimu, akisema hatua hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha mazingira ya kazi na mafanikio yao kitaaluma.

Katika hotuba yake, Mwalimu Pantaleo amewasilisha maombi mawili kwa Balozi Chen ili kuimarisha ushirikiano kati ya walimu wa jiji la Arusha na China.

“Ombi letu la kwanza ni kuomba ufadhili wa masomo ya elimu ya juu nchini China kwa walimu wa jiji la Arusha. Ombi la pili ni kutuunganisha na jiji rafiki nchini China ili walimu wa majiji haya waweze kubadilishana uzoefu,” amesema Pantaleo.

Hafla hiyo, iliyofadhiliwa na Ubalozi wa China na kampuni ya Oryx Gas, imeratibiwa na Mbunge Mrisho Gambo kama sehemu ya juhudi za kuunga mkono Kampeni ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, ambayo inalenga kupunguza matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa katika kaya za Tanzania.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *