Mkazi wa barabara ya nne jijini Tanga aliyetambulika kwa jina la Bagidad (60) mwenye asili ya kiasia ambaye mke wake alikutwa amenyongwa pamoja na mfanyakazi wake na yeye amekutwa amekufa baada ya mwili wake kuokotwa katika eneo la Nguvumali B jijini Tanga.
Mwili wa mtu huyo umekutwa katika eneo hilo lenye pori ambapo mpaka sasa bado haijajulikana chanzo cha kifo chake.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema waligundua tukio hilo baada ya kusikia harufu kali iliyokuwa ikitokea eneo ambalo amekutwa amekufa na hivyo kuwalazimu kujua ni kitu gani kilichopelekea harufu hiyo na ndipo walipokutana na mwili huo.
Mjumbe wa mtaa wa Nguvumali B amesema ndani ya siku mbili mfululizo alikuwa akikutana na harufu hiyo akiamini ni mizoga ya wanyama ambayo imekuwa ikitupwa na wafugaji.
“Polisi walikuja wakaangalia wakawapigia simu ndugu zao wamekuja kuhakikisha kama kweli huu mwili ni wa ndugu yao wakakiri kuwa ni ndugu yao na ndipo taratibu nyingine zikaendelea kwajili ya kuuhifadhi mwili huo, “alisema mjumbe huyo wa serikali ya mtaa.
Akizungumza Bongo news TV, Diwani wa kata ya Nguvumali Mustapha Selebosi ameelezea namna walivyoweza kuutambua mwili huo na kueleza kuwa walimuona mbwa akitokea kwenye eneo alilokuwepo marehemu ambapo baada ya kufuatilia walikuta mwili huo.
“Tulianza kujiridhisha kwenyd hatua za awali moja utanashati ambao yule bwana alikuwa nao, inavyoonekana sio kama mtu aliyenyongwa au aliyeuliwa kwenye eneo hili mwili huu ulikuwa umezongwa na wadudu waharibifu, “alisema Selebosi.
Hata hivyo Jeshi la polisi halikuweza kutolea ufafanuzi suala hilo kutokana na Kamanda wa polisi Mkoa Tanga Almachius Mchunguzi kuwa kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa.
Katika taarifa ya awali jeshi la polisi lilimuhusisha marehemu na kifo cha mke wake pamoja na mfanyakazi waliokutwa wamenyongwa na kutobolewa macho nyumbani kwao barabara ya nne jijini Tanga.