Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Bajeti imeeleza kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kukusanya Kodi, kuhudumia wateja na kutoa elimu ya Kodi kwa Wananchi.
Akiwa katika mafunzo yaliyoandaliwa na TRA kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Oran Njeza amesema Elimu ya Mlipakodi inayotolewa na TRA imewafikia watu wengi hali ambayo imepunguza vitendo vya ukwepaji wa Kodi miongoni mwa wafanyabiashara.
Mhe. Njeza amesema TRA inapaswa kuongeza wigo wa kukusanya mapato kwa kutafuta vyanzo vipya vya kodi na kupunguza viwango vya kodi huku akishauri kuwekeza zaidi katika mifumo ya TEHAMA itakayosaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi maana mifumo itaweza kusomana.
Nao baadhi ya Wabunge waliochangia wakati wa mafunzo hayo ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo Dk. Charles Kimei na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Shally Raymond wameshauri kutazamwa zaidi kwa sekta za uzalishaji na Sheria zake ikiwemo Utalii, Madini na Kilimo.