Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, amepongeza Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kwa mchango wao mkubwa katika kutoa maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akieleza matumaini kwamba rasimu hiyo inaleta mwanga wa mabadiliko chanya kwa watu wenye ulemavu nchini.

Akizungumza katika mkutano wa kuhakiki rasimu hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Jumapili tarehe 15 Desemba 2024, Naibu Waziri Ummy ambaye ni mgeni rasmi katika mkutano huo amesema uandaaji wa Dira ya Maendeleo 2050 umezingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu kwa kiwango kikubwa.

“Tunaona uandishi wa dira hii umezingatia masuala ya watu wenye ulemavu katika kiwango chake bora. Nakala hii, miaka 25 ijayo, inatupa matumaini kwamba mambo ya watu wenye ulemavu hayatakuwa ya kutafuta tena bali yatakuwa wazi na yaliyowekwa moja kwa moja,” amesema Naibu Waziri.

Naibu Waziri Ummy ameeleza kuwa Dira hiyo imeweka msisitizo mkubwa katika utoaji wa elimu kwa watu wote, hatua inayolenga kuondoa ubaguzi na kuhakikisha makundi yote, yakiwemo ya watu wenye ulemavu, yanapata maarifa na ujuzi wa kujikwamua kimaisha. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye tafiti ambazo zitatumika kuandaa sera na kufanya maamuzi yatakayosaidia kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu.

“Tufanye maamuzi kwa kutengeneza sera, sheria, na miongozo ambayo itasaidia kupeleka mbele kundi letu la watu wenye ulemavu,” ameongeza Naibu Waziri.

Katika hotuba yake, Naibu Waziri ameishukuru Timu ya Uandaaji wa Dira ya 2050 kwa kuzingatia maoni ya watu wenye ulemavu na kuahidi kuwa kundi hilo litaendelea kushirikiana kikamilifu kuhakikisha dira hiyo inakamilika kwa mafanikio.

Naibu Waziri amerejea pia mkutano wa awali wa tarehe 16 Agosti 2024, ambapo watu wenye ulemavu walijitokeza kutoa maoni yao juu ya kupunguza umasikini, kujengewa uwezo wa kiuchumi, na kuimarisha usawa wa kijinsia kwa makundi maalum kama vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *