Baadhi ya Walipakodi mkoani Arusha wameshangazwa na kitendo cha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Mwenda kuwatembelea katika shughuli zao na kuwashukuru kwa kulipa Kodi vizuri huku akiwakabidhi zawadi na kusikiliza changamoto zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya Walipakodi hao akiwemo Satbir Singh Hanspaul ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Hanspaul inayounda magari ya kubebea watalii amesema ni mara ya kwanza kutembelewa na kiongozi wa ngazi ya juu wa TRA jambo ambalo litawapa morali zaidi ya kulipa kodi na kuchangia pato la Taifa.
Mkurugenzi huyo amesema katika kipindi cha karibuni kumekuwa na mazingira rafiki ya ukusanyaji kodi yanayotoa ahueni kwa mlipakodi kutokana na kuwepo kwa utaratibu wa kusikilizwa pale panapotokea changamoto katika mazingira yao ya kazi.
Naye Mkurugenzi wa Miradi World Vision Tanzania Bi. Nesserian Mollel amesema shughuli wanazofanya zinaisaidia jamii ya Tanzania mijiji na bijijini na wamekuwa wakilipa kodi kwa uaminifu hata kwa mizigo wanayoingiza nchini kutoka kwa wahisani nje ya nchi kwaajili ya kuwasaidia watanzania.
Amesema kutembelewa na Kamishna Mkuu wa TRA kumewapa motisha ya kuendeleza uaminifu katika kulipa kodi na kuwa wataitumia vizuri fursa ya mazungumzo na TRA ili wapate ahueni ya kodi.
Mwakilishi wa Kampuni ya kuzalisha mbegu ya Enza Zaden Africa Gerald Matowo ambaye ni Meneja uendeshaji amesema wanajivunia kuwa walipakodi wazuri waliotambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA na kuwa wataendeleza uaminifu huo.
Kamishna Mkuu wa TRA yupo ziarani katika mikoa mbalimbali nchini kutoa Shukurani kwa Walipakodi na kuwasikiliza.