NA Mwandishi Wetu
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amekemea vitendo vya ubabaishaji na rushwa miongoni mwa watumishi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) akisema vinaweza kufuta mazuri yote ambayo taasisi hiyo imeyafanya na inaendelea kuyafanya.
Akizungumza na Menejimenti ya TEMESA na Mameneja wa Mikoa jijini Dodoma, Waziri Ulega ameeleza Serikali imedhamiria kuifanya TEMESA kuwa taasisi namba moja na kimbilio la wote katika utengenezaji wa magari ya Serikali na binafsi.
“Tunatakiwa kupiga vita sana vitendo vya ubabaishaji na rushwa. Huu ndiyo ugonjwa unaoharibu taasisi nyingi na kwa kweli tunahitaji kutumia uwezo wetu wote kupambana na jambo hili,” alisema.
Huo ulikuwa ni mkutano wa kwanza baina ya Waziri Ulega na viongozi wa TEMESA tangu ateuliwe kuwa waziri wa wizara hiyo mwezi huu.
“Hongereni kwa kuanzisha mkakati wa mpya wa kufanya kazi utakaowawezesha kujiendesha kibiashara kwa kushirikiana na sekta binafsi pale inapobidi ili kuihudumia jamii kikamilifu. Sisi TEMESA ni lazima tuwaoneshe watu ukinilipa nitakufanyia kazi kwa wakati”, amesema Ulega.
Amezipongeza Taasisi za BOT, EWURA, TANESCO na TRA kwa kulipa madeni yao kwa wakati na kupewa huduma kwa haraka na kuzitaka taasisi nyingine za Serikali kuweka mikataba ya huduma bora na za haraka na TEMESA ili kusaidia taasisi hiyo kuondokana na madeni.
Waziri Ulega ameeleza kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni 67.4 zimetumika katika miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga vivuko vipya sita (6), ukarabati wa vivuko saba (7) na ujenzi wa miundombinu ya vivuko ambayo ni maegesho na majengo ya abiria katika Ziwa Victoria na Bahari ya Hindi.
Waziri huyo aliutumia mkutano huo kupongeza ukarabati wa karakana za matengenezo ya magari unaoendelea kufanyika kote nchini na kusisitiza ukarabati huo uendane na mabadiliko ya kimtazamo, utaalamu na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ili kuleta tija na ufanisi katika majukumu yao.
Naye, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Charles Msonde, amezungumzia umuhimu wa taasisi za Wizara ya Ujenzi kushirikiana kwa kubadilishana uzoefu ili kuleta ufanisi unaotarajiwa kwa Wananchi na taifa kwa ujumla.