Mwanaharakati wa Haki za Binadamu nchini Tanzania, Maria Sarungi , amehojiwa na kituo cha Televisheni cha NTV, Kenya, na kuelezea namna alivyotekwa na watu wasiojulikana.
Taarifa za Maria kutekwa zilisambaa jana Jumapili, Januari 12, ambapo baadaye jioni Maria alijitokeza na kusema watekaji wamemuachia na yupo salama.
“Nipo salama nitazungumza kesho”alisema
Katika mahojiano na kituo hicho leo, Maria, amesema, watu waliomteka walikuwa wanne, watatu ndio walioshuka kwenye gari baada ya kumteka na walikuwa wakizunguka zunguka.
“Mwisho kabla hawajaniachia, dereva pia alishuka, nikabaki na mtu wa kulia kwangu, aliyekuwa amenikaba amenishikilia, hakushuka nje ya gari muda wote, nadhani alikuwa ndiye alipewa jukumu la kunilinda,”amesema
Maria ameeleza kuwa, mara baada ya dereva wa gari hilo kushuka, alitumia muda mrefu kabla ya kurudi kwenye gari.
“Nadhani labda walikuwa wakitafuta ushauri, kulikuwa na mtu aliyekuwa akizungumza Kiswahili, nahisi alikuwa akipokea maagizo na nilikuwa nahisi wanatumia lugha ya alama kuwasiliana ili nisiwaelewe,” amesema.