WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, amewataka wazazi na walezi wasiwafiche watoto wenye ulemavu na wahakikishe wanafahamika mahali walipo, hali zao za ulemavu ili waweze kupata huduma stahiki na washiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 25, 2025), wakati akizindua Kanzidata na Mfumo wa Taarifa za Watu Wenye Ulemavu unaotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amezitaka taasisi zote zinazotoa huduma kwa watu wenye ulemavu watumie takwimu hizo katika kutayarisha programu za kuwawezesha na kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo kujiendeleza kiuchumi, kijamii na mazingira.

“Taasisi zote za umma, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo washirikiane na Serikali kutumia mfumo huo kikamilifu kwa kufanya maamuzi yenye vigezo vya kitakwimu katika kupanga na kufuatilia utekelezaji wa sera, mipango na afua mbalimbali zinazolenga kukuza na kuimarisha maendeleo ya watu wenye ulemavu.”

Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote nchini wahakikishe Ofisi za Ustawi wa Jamii katika halmashauri zote nchini zinatekeleza wajibu wa kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi wenye ulemavu,.

“Watekelezaji na wasimamizi wa miradi mbalimbali ya ujenzi wahakikishe uwepo wa miundombinu fikivu kwa ajili ya watu wenye ulemavu.”

Akizungumzia kuhusu matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, amesema asilimia 11.2 ya watu wote nchini wana ulemavu wa aina fulani, idadi hiyo imeongezeka kutoka asilimia 9.3 ilivyokuwa katika Sensa ya Mwaka 2012.

Akielezea kuhusu juhudi za kuimarisha ustawi wa watu wenye ulemavu nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ustawi bora wa jamii ya watu wenye ulemavu ikiwemo kutunga na kutekeleza sera, sheria na programu mbalimbali za kulinda haki, fursa na maendeleo ya Watu wenye Ulemavu.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *