Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amewasihi viongozi wa ngazi mbalimbali mkoani humo na nchi kwa ujumla kuendelea kutoa haki kwa watu bila upendeleo wowote wa kiimani, hali na itikadi na hadhi ya mtu, akiongeza kuwa nchi ya Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa haki za binadamu licha ya changamoto ambazo zimeendelea kuwepo.

RC Mtanda ameyasema hayo siku ya Jumanne Februari 18, 2025 alipomwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria kama ugeni rasmi, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) mkoani humo uliofanyika katika Uwanja wa Furahisha.

Ameeeleza kuwa maendeleo ya jamii hayataweza kufikiwa kama hakutakuwa na haki na amani akitolea mfano mataifa yenye migogoro ya ndani ambayo imesababisha raia wao kuhama na namna maendeleo yamekuwa duni katika mataifa hayo.

“Hakika kundi la wananchi wanyonge, wanaoishi pembezoni, ambao si rahisi kupata msaada wa kisheria na wasio na uwezo litakuwa limefikiwa kwa kiwango kikubwa, na wengi sasa hawatapoteza muda mwingi kushughulikia changamoto zao za kisheria bali watajikita katika shughuli za maendeleo”, ameeleza Mtanda.

Halikadhalika amesema kupitia kampeni hiyo Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ana imani kuwa elimu na huduma za kisheria zitakazotolewa, watendaji wa serikali pamoja na wananchi watapata uelewa wa masuala ya kisheria na kutatuliwa migogoro inayowakabili kwa urahisi na ufanisi bila malipo.

Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Alfredy Dede amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imelenga kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wakati hususani kwa wananchi wanyonge na katika mkoa wa Mwanza, kampeni itafanyika katika wilaya zote, kata, mitaa na vijiji kwa muda wa siku 10.

Katika kuhakikisha lengo hilo linatimia, kazi kubwa itakayofanyika ni kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kisheria, utawala bora, elimu kuhusu mapambano ya ukatili wa kijinsia, usimamizi wa mirathi na urithi, haki za ardhi, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, haki za binadamu na wajibu, yakiwemo masuala muhimu katika ndoa.

Aidha amesema kampeni hiyo itahusisha pia elimu ya katiba na uraia kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ikiwamo Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya, madiwani na wakurugenzi.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Sheria Tanganyika (TLS) kwa niaba ya Baraza la Uongozi la chama hicho Boniface Mwabukusi amesisitiza upendo, utu na utii katika jamii akieleza vitu hivyo vitatu vikiwepo basi migogoro ya ardhi, ndoa na mirathi itakuwa ni historia katika jamii.

“Kama taifa, bila kujali nafasi ya mtu aliyopo lazima jambo la kwanza na msingi mkuu uwe ni Ibara ya 9 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozungumzia utu, upendo na utii katika kitafsiri sheria”, ameeleza Mwabukusi.

Yassin Ali, Mwenyekiti wa Kamati ya Msaada wa Kisheria mkoa wa Mwanza ambaye pia Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Kivulini ameiomba Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya Ndani kuwezesha uwepo wa siku ya msaada wa kisheria ya kitongoji, kijiji na kata ili jitihada zinazofanywa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ziwe endelevu kwa huduma ya msaada wa kisheria iendelee kuwafikia wananchi wa pembezoni.

Naye mwakilishi wa Mashirika ya Watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria mkoa wa Mwanza Matoke Jackson amesema mashirika hayo yanaaahidi kutoa huduma hiyo ya kisheria kwa ufanisi kwa kuzingatia mwongozo wa kampeni husika, na sheria na kanuni za Msaada wa Kisheria.

Tangu kuzinduliwa kwa Kampeni hiyo mwaka 2023, jumla ya mikoa 17 imefikiwa na kuzinduliwa kwa kampeni hii mkoani Mwanza jumla ya mikoa itakuwa ni 18 ambayo inahusisha Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma, Simiyu, Singida, Njombe, Iringa, Njombe, Mara, Songwe, Morogoro, Kigoma, Katavi, Mtwara, Tabora, Geita, Kilimanjaro. Halikadhalika kampeni hiyo inatarajiwa kuendelea katika wilaya zote nane za mkoa wa Mwanza.

About Author

Bongo News

1 Comment

    Your content is magnificent, it’s no wonder you have such a readership.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *