▪Awataka waumini kuutunza msikiti huo
▪Atoa wito kwa viongozi wa dini kuliombea Taifa na kukemea maovu
 
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Machi 14, 2025 amezindua msikiti wa Masjid Jaami’u Nuuril Hikma uliopo mtaa wa Yombo, Temeke jijini Dar es Salaam ambao umejengwa na Taasisi ya Al-Hikma.


Akizungumza baada ya kuzindua msikiti huo, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa jamii na Watanzania watakaotumia msikiti huo kuutunza kwani kufanya hivyo ni njia ya kudumisha uhusiano na Mwenyezi Mungu na inahesabika kama sadaka.


“Mtume Muhamad S.A.W anatufundisha pia kutunza nyumba za ibada, msikiti ni sehemu ya jamii na ni mahali pa ibada na umoja. Kupitia hadithi ya Bukhari, ni wajibu wa waumini kutunza msikiti, kuhakikisha kwamba ni sehemu safi, na inakidhi mahitaji ya ibada na mafunzo ya kiislamu.”


Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa msikiti ni kituo cha kiroho, kijamii, kiutamaduni na nyumba kwa ajili ya ibada na unatoa nafasi kwa waumini kushirikiana katika ibada, kujifunza, na kujenga jamii bora kwa kutoa huduma za kijamii.


Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini kuliombea Taifa pamoja na kukemea vitendo vyote visivyo mpendeza Mwenyezi Mungu.


“Tunajua mnaliombea Taifa hili, ila endeleeni kufanya hivyo ili utulivu huu uendelee, tuachane na mambo yatakayoleta adha kwenye jamii, tunafurahi mnavyohubiri amani na mshikamano, Mwenyezi Mungu analipenda Taifa hili.”


Pia Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa ujenzi wa msikiti huo. “Ujenzi wa Msikiti huu ni ishara ya juhudi za taasisi hii katika kuimarisha misingi ya imani na maadili mema katika jamii”.


Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt Abubakar Zuber Ali Mbwana amesema kuwa maendeleo sio ugomvi bali ni kufanya mambo yanayoonekana na  yanayompendeza Mwenyezi Mungu ikiwemo ujenzi wa msikiti “fitna, ugomvi, fujo kwenye misikiti hatutaki, tupendane na heshima itawale.”

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *