Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Sheikh Ally Hamis Ngeruko ametoa wito kwa Watanzania kuwarithisha Watoto wao utamaduni wa kulipa Kodi kwa hiari ili watakapokuwa watu wazima wawe Walipakodi wazuri na kujenga nchi.

Ametoa rai hiyo Machi 14.2025 katika hafla ya Iftari iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Jijini Dar es Salaam.

Sheikh Ngeruko amesema nchi haijengwi kwa udongo bali kwa mapato hivyo Watoto wakijengewa utamaduni wa kulipa Kodi kama ilivyo kwa wazazi wao nchi itaendelea kujengwa ambapo pia amehimiza ulipaji Kodi kwa hiari na kwa uaminifu.

Kwa upande wake
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema kila mmoja akilipa Kodi kwa hiari matokeo ya Kodi yataongezeka.

“Tumekaa hapa ukumbini kwa amani kwa sababu kuna ulinzi na usalama, hayo ni matokeo ya kodi, kila mmoja amefika hapa kwa kupita barabarani nazo zimejengwa kwa kodi, Elimu bure inayotolewa kwa Watoto wetu nayo ni matunda ya kodi hivyo tuendelee kuchangia katika kulipa Kodi ” amesema Mwenda.

Kamishna Mkuu Mwenda ametoa wito kwa Waislamu na Wakristo nchini katika kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadan na Kwaresma, ambapo matumizi ni makubwa, wadai risiti kwa kila wanapofanya manunuzi ili kuisaidia nchi.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema kuwa Watumishi wa TRA wataendelea kutenda Haki katika kutoza kodi kwa kutochukua wasichostahili na kutokiacha wanachostahili na kuwaomba Walipakodi waendelee kulipa Kodi kwa hiari.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *